SIMULIZI: SHADIA (LAANA INAYOTEMBEA)
MTUNZI: SUMAIYA MWENDO TUPO HAPA. COM
SEHEMU YA: 41
ENDELEA.................
Shadia alikuwa ameshikilia simu yake kwa mkono uliojaa wasiwasi, vidole vikitetemeka. Akijaribu kupata utulivu wa nafsi, alibonyeza namba za Bwana Saleh. Hakukuwa na mtu mwingine wa kumtegemea. Lakini kabla hajachukua hatua ya kuongea, mkono wa Yasri, dhaifu lakini wenye nguvu ya kumshawishi, ulimzuia.
“Usipige... tafadhali,” Yasri alisema kwa sauti iliyovunjika, akitikisa kichwa. Macho yake yalionyesha hofu na ombi zito.
Shadia alisimama pale, moyo wake ukigawanyika kati ya woga na huruma. Alimtazama Yasri, damu ikiendelea kutiririka kutoka kwenye jeraha lake. Hakuwa na ujuzi wa daktari. Hakujua afanye nini zaidi ya kuogopa.
Akiwa bado kwenye mshangao huo, mlango wa chumba ulikuwa ukigongwa kwa nguvu ya kutisha. Shadia alitetemeka, mwili wake ukionekana kufa ganzi. Alitembea kwa taratibu kuelekea mlangoni, akiweka sikio lake karibu, akihisi hofu ya kutaka kumgundua aliyekuwa upande wa pili.
“Ni nani?” aliuliza kwa sauti ya chini iliyojaa hofu.
“Sima na Sultana,” sauti ya Sima ilijibu kutoka nje ya mlango.
Shadia alifungua mlango taratibu, na hapo alikuta uso wa Sultana, akionekana mwenye tahadhari lakini aliyedhamiria. Sima alikuwa nyuma yake, akitazama kwa wasiwasi.
Shadia alihisi mshituko. Yasri hakuwa tayari mtu yeyote ajue hali yake, lakini Sultana alisukuma mlango na kuingia kwa nguvu, bila kusita hata kidogo.
“Sultana! Hapana!” Shadia alisema kwa ukali, akimfata nyuma.
“Huna uwezo wa kunizuia, Shadia,” Sultana alisema kwa sauti thabiti, akimkazia macho. “Kama hujui, mimi ndiye pekee niliye na uwezo wa kumrudisha Yasri kwenye hali yake. Ukisubiri zaidi, utampoteza.”
Maneno hayo yaliangukia moyoni mwa Shadia kama mshale wa moto. Alimtazama Sultana kwa mshangao na mashaka, lakini kulikuwa na ukweli kwenye sauti yake. Hakukuwa na muda wa kubishana.
Shadia aligeuka na kumwambia Sima, “Rudi, Sima, nitakueleza baadaye kila kitu. Tafadhali ondoka.”
Sima alijaribu kuhoji, lakini sura ya Shadia ilimshinda. Aliondoka kimya kimya huku Shadia akifunga mlango nyuma yake kwa haraka na kurudi ndani.
Sultana tayari alikuwa akifungua begi lake, akitoa zana za kienyeji. Alikuwa na majani makavu, viungo vya ajabu, na nyuzi za aina mbalimbali. Shadia aliganda aliposhuhudia.
“Hivi... umetoka navyo wapi?” Shadia aliuliza, sauti yake ikiwa na mshangao wa wazi.
“Yasri aliniamini kabla yako, Shadia, kuwa na subra,” Sultana alisema, akimkazia macho huku akiendelea kuandaa dawa zake.
Wakati huo, Yasri alifumbua macho kwa sekunde chache tu alipomuona Sultana. Lakini kabla hajazungumza, alizimia kabisa, mwili wake ukiangukia kitandani bila nguvu.
“Yasri!” Shadia alipiga kelele kwa hofu, machozi yakitiririka mashavuni mwake. Alikuwa karibu kuishiwa nguvu.
“Lia ukitaka, lakini Utahitajika kunisaidia,” Sultana alisema kwa ukali. “Nenda ukachemshe maji ya moto. Haraka!”
Shadia, akiwa kama mtu aliyepoteza akili, alikimbilia bafuni na kuwasha jagi la maji ya moto. Mkono wake ulitetemeka alipokuwa
akifungua bomba la maji. Akijaribu kutoanguka, alichemsha maji huku mawazo yakiwa mazito.
Aliporejea chumbani na sufuria ya maji ya moto, alimkuta Sultana akijitayarisha kusafisha jeraha la Yasri. Shuka za kitanda tayari zilikuwa zimelowana kwa damu, na harufu ya chuma (risasi) ilijaa hewani.
“Leta shuka lingine, na ulete taulo safi,” Sultana aliamuru bila hata kumtazama Shadia.
Shadia alitii, akiharakisha hata wakati hofu ilipomuelemea. Sultana alionekana hana woga, macho yake yakiwa thabiti huku akianza kazi yake.
“Una uhakika... utaweza kumsaidia?” Shadia aliuliza, sauti yake ikiwa dhaifu.
“Kama hutaki kuona akifa mbele yako, niache nifanye kazi yangu,” Sultana alijibu bila hisia, akianza kuosha jeraha kwa maji ya moto.
Shadia aliweka mkono mdomoni, akizuia kilio chake, huku akimshuhudia Sultana akifanya kazi kwa ustadi wa kushangaza. Hofu ilikuwa nzito, lakini kilichokuwa kinamsukuma Shadia kilikuwa matumaini madogo kwamba Yasri angerejea tena kwenye hali yake ya kawaida.
Sultana alichukua mshumaa wake na kuuwasha. Nuru ya mwanga wake ilicheza na vivuli vya chumba, ikiongeza mvutano wa kila tukio. Kisu kidogo kiliinuliwa mkononi mwake, na kwa
taratibu, alikikabidhi kwa mwanga wa mshumaa. Moto uliendelea kukilamba mpaka kisu kikageuka chekundu kama lava ya volkano.
Shadia alikuwa amesimama pembezoni, mwili wake ukitetemeka kana kwamba alikuwa ndani ya tundra. Alimtazama Sultana, hofu ikionekana wazi usoni mwake. “Unapanga kufanya nini?” aliuliza kwa sauti iliyokatika, lakini Sultana hakujibu, macho yake yakiwa yameelekezwa kwa Yasri.
“Kama huwezi kuvumilia, basi funika macho yako,” Sultana alisema kwa ukali, huku akiweka kisu karibu zaidi na jeraha la Yasri.
Shadia alitetemeka zaidi. “Fumba macho?” alijirudia kimoyomoyo. Hapana, hawezi
kuamini kile Sultana anafanya kwa Yasri bila kushuhudia. Hata hivyo, alihisi miguu yake ikilegea.
"Mzibe mdomo, haraka!" Sultana aliamuru.
Kwa mkono uliojaa wasiwasi, Shadia aliuziba mdomo wa Yasri, mikono yake ikiwa na jasho la hofu. Alijaribu kuyaepuka macho ya Yasri, aliekuwa akitetemesha nyusi kwa maumivu, lakini hakuweza. Yasri alionekana kujiandaa kwa mateso.
Sultana, bila huruma, alizamisha kisu kile cha moto kwenye jeraha la kwanza. Yasri aliruka kwa maumivu, mwili wake ulitetemeka kwa nguvu. Shadia alihisi mwangwi wa kilio chake umezibwa na mikono yake, lakini bado alipiga
kelele kwa hofu. Ilikuwa kama maumivu ya Yasri yalihamia kwake. Ilhali aliuziba mdomo wa Yasri ili asipige kelele lakini yeye ndo alipiga kelele.
“Kaza, Shadia!” Sultana alisema kwa sauti thabiti, bila kuonyesha hisia zozote. “Hii ni njia pekee ya kuokoa maisha yake.”
Kisu kilitoka, na pamoja nacho, risasi ya kwanza ilianguka chini kwa sauti ndogo lakini ya kutisha. Yasri alitulia kwa sekunde, lakini maumivu hayakuisha. Na vile aliingiziwa kisu bila ganzi, maumivu yake hayakuvumilika.
Sultana alijitayarisha tena. “Kuna moja zaidi,” alisema kwa sauti iliyopoa, kana kwamba hiyo ilikuwa kazi ya kawaida kwake.
Shadia hakutaka kuona zaidi. Machozi yalitiririka mashavuni mwake bila kujizuia. Alihisi kama muda ulikuwa umesimama, kila sekunde ikijaa mateso. Risasi ya pili
iliondolewa kwa ustadi uleule, lakini wakati huu, Shadia hakuweza kujizuia; alijikuta ameketi sakafuni, akihema kwa shida, macho yake yakikwepa damu iliyokuwa ikitiririka.
Sultana alichukua maji ya moto na dawa, akaosha kidonda cha Yasri kwa umakini wa ajabu. “Hii itazuia maambukizi,” alisema kwa sauti iliyotulia, kana kwamba hakujali hali ya Shadia aliyekuwa amejaa hofu na kuchanganyikiwa.
Baada ya kazi yake kumalizika, Sultana alinyanyuka, alifunga begi lake na kumkabidhi Shadia chupa ya dawa. “Hakikisha unampa dawa hizi kwa wakati. Ataamka tu. Kazi yangu imekwisha.”
Shadia hakuweza kusema chochote. Alikuwa bado amezama kwenye mshtuko. Sultana, kama kwamba hakutokea chochote, alitoka nje ya chumba, akimuacha Shadia na Yasri kwenye hali ya ukimya mzito.
Shadia alipotazama damu iliyokuwa imemwagika sakafuni, alihisi kama alikuwa akizama kwenye ndoto mbaya isiyokwisha. Aliinuka na kuanza kusafisha sakafu kama mtu aliyepoteza akili, macho yake yakiwa hayana mwelekeo. Jasho lilikuwa likitiririka usoni mwake, huku damu ikiendelea kumtisha.
Lakini ghafla, mlango ulifunguliwa tena. Sultana alirudi kwa haraka, uso wake ukiwa hauna hisia. Bila kusema chochote, alichukua begi la Yasri lililokuwa pembeni ya kitanda. Shadia alisimama, akiangalia kwa mshangao.
“Nani kakuambia ulichukue hilo begi?” Shadia aliuliza kwa sauti dhaifu.
Sultana hakujibu. Alifungua begi hilo, na kwa haraka akatoa mafungu ya pesa nyingi, zilizofungwa kwa uangalifu.
Shadia alipigwa na butwaa. “Hizo pesa zote... Yasri katoa wapi?” aliuliza, sauti yake ikitetemeka.
“Hilo si la muhimu kwako, Shadia,” Sultana alisema kwa ukali, akifunga begi hilo na kuondoka.
Lakini Shadia hakubaki kimya. Akiwa amesimama pale, akili yake ilianza kuunganishwa. Alikumbuka jinsi Yasri alivyoruka fensi, alivyoonekana mwenye wasiwasi, na jinsi alivyokuja na jeraha. Mawazo yake yalimsukuma kwenye hitimisho moja tu— pesa hizo, huenda Yasri aliziiba.
Alishika mdomo wake kwa mikono miwili, machozi yakianza kumtiririka tena. “Haiwezekani,” alijisemea kimoyomoyo, akimtazama Yasri aliyelala kitandani bila fahamu. “Siwezi kuamini Yasri ni mwizi??...”
Lakini hata hivyo, ukweli ulikuwa unazidi kumkaba. Yasri alihusika kwenye jambo zito, na sasa hakuwa na pa kukimbilia tena. Zaidi ya kulala kitandani kama marehemu mtarajiwa.
SOMA MAELEKEZO
Bonyeza hi "Soma Kitabu" kisha itakupeleka kwenye fomu yaku login, hakikisha ume login na namba uliyojiunga nayo ndipo utaendelea sasa kusoma kitabu chote