SHADIA (season 2)

book cover og

Utangulizi

SIMULIZI: SHADIA (LAANA INAYOTEMBEA)
MTUNZI: SUMAIYA MWENDO TUPO HAPA. COM
SEHEMU YA: 21
ENDELEA............
Yasin alipomtazama Shadia akiwa amelala, uso wake ulionekana kuwa na utulivu wa kipekee. Akiwa bado amesimama mlangoni, aliingiwa na hisia tofauti, lakini kabla hajafikiria zaidi, Sima aliingia ghafla na kumuita Shadia. Sauti yake ya upole ilimfanya Yasin aghaflike kidogo na kujiondoa pale kimyakimya bila kusema neno.
Sima alimtazama Yasin akiondoka, kisha akatabasamu kwa namna alivyokuwa mtulivu na

mpole. Alimkaribia Shadia na kwa upole akamgusa begani.
“Shadia...amka kidogo. Chakula kipo mezani, hujapata chochote tangu umekuja,” Sima alisema huku akimsaidia Shadia kuinuka.
Shadia alifumbua macho kwa uvivu, mwili wake ukiwa bado na uchovu.
“Asante, lakini sijisikii njaa sana,” alisema kwa sauti ya chini.
“Ni lazima ule. Mwili wako unahitaji nguvu. Njoo, nitakusaidia kutembea,” Sima aliongeza kwa msisitizo, huku akimnyanyua kwa upole.
Walipofika sebuleni, Sima alimtengea chakula kwenye sahani safi, kisha akaweka mezani mbele yake.

“Haya, kula. Chakula ni baraka,” Sima alitabasamu kwa ukarimu.
Shadia alikitazama chakula hicho kwa muda, macho yake yakiwa yamejawa na kumbukumbu za mama yake. Ukarimu wa Sima ulimkumbusha jinsi mama yake, Bi Maimuna, alivyokuwa akimhudumia alipokuwa mdogo hadi umri huo. Kwa muda mfupi, macho yake yalilowa na hisia, lakini alifuta machozi kwa haraka ili asionekane dhaifu.
“Pole, naitwa Sima. Wewe unaitwa nani?” Sima alimuuliza kwa utulivu.
“Naitwa Shadia,” alijibu kwa sauti ya upole, huku akiendelea kula.

Dakika chache baadaye, sauti ya hatua ilisikika ikikaribia. Alipoinua macho, alimwona Yasin akija upande wao, alikuwa amevalia mavazi mepesi ya nyumbani. Alikuwa amevaa fulana nyeupe na suruali ya kitambaa laini, mwonekano wake ukiwa wa kawaida lakini wa kupendeza. Alikuwa mtulivu kama kawaida, akielekea moja kwa moja mezani na kuketi karibu na Shadia.
Shadia alimwangalia Yasin kwa woga wa ndani, lakini macho yake hayakuweza kuacha kumtazama. Alijihisi tofauti, moyo wake ulidunda kwa kasi isiyo ya kawaida. Yasin hakuwa na maneno mengi, na ukimya wake uliongeza uzito wa uwepo wake.
“Hujambo?” Yasin aliuliza kwa sauti ya chini, huku akichukua kikombe cha maji.

“Sijambo... asante,” Shadia alijibu kwa sauti iliyokuwa karibu na kunong’ona, macho yake yakishindwa kumwangalia moja kwa moja.
Sima, aliyekuwa pembeni, alitabasamu kwa furaha ya siri alipowaona.
“Nikihitaji chochote, nitakuwa jikoni,” Sima alisema, kisha akaondoka na kuwaacha peke yao.
Ukimya ukatawala mezani. Kila mmoja alikuwa bize na chakula chake, lakini Shadia aliweza kuhisi joto la uwepo wa Yasin karibu naye. Ingawa hakuwa akizungumza, utulivu wake ulikuwa wa kuvutia, na kila mara macho yao yalipokutana kwa bahati, Shadia alihisi moyo wake ukitetemeka kidogo.

Mlo ulipoisha, Shadia alijikuta akijiuliza maswali mengi kuhusu Yasin. "Kwa nini hakuongea zaidi? Na kwa nini moyo wake ulionekana mzito licha ya kutabasamu mara chache?" Hali hiyo ilimfanya ahisi kuvutwa zaidi na mtu huyo wa ajabu.
Shadia na Yasin wakiwa bado mezani wanakula chakula kwa utulivu, mlango wa sebuleni ulifunguliwa ghafla, na Bi Leila akaingia huku akiwa ameshikilia simu sikioni. Sauti yake ya ukali ilitawala sebuleni.
“Sikuelewi kabisa! Mlipaswa kuwa mmekamilisha kazi wiki iliyopita, sasa hizo kuta kupasuka zimetoka wapi? Sijali majibu yako, nataka kila kitu kirekebishwe haraka iwezekanavyo!” alisema kwa hasira, akitembea huku na huko.

Baada ya kumaliza mazungumzo, alikata simu kwa ukali na kupumua kwa nguvu, kisha akatulia kidogo kabla ya kuelekea mezani. Bila hata kuangalia vizuri, aliketi kwenye kiti karibu na Shadia na Yasin.
“Niletee maji ya kunywa,” alisema kwa sauti ya amri, huku akimgeukia Shadia bila kufikiria kwamba msichana huyo alikuwa mgeni.
Shadia alimtazama kwa mshangao, macho yake yakieleza kutokuamini. Alisimama polepole, akiwa hana hakika ni wapi angepata maji. Akajaribu kukumbuka alipoona Sima akitoka, na kwa haraka aliamua kufuata mlango uliomuongoza jikoni.

Akiwa jikoni, alikuta jagi la maji na kikombe vilivyopangwa kwa usafi kwenye meza. Alimimina maji kwa uangalifu, kisha akarudi sebuleni huku akihisi macho ya Bi Leila yakimfuatilia. Alimkabidhi maji kwa adabu zote.
“Asante,” Bi Leila alisema kwa sauti isiyo na shukrani dhahiri. Shadia akarudi kuketi, akijikunyata kwa aibu. Hakuwa na mahali pengine pa kwenda, hivyo alikaa kimya.
Bi Leila akamtazama kwa makini, kisha kwa sauti ya upole lakini yenye lawama akasema, “Hivi wewe, mfanyakazi wa ndani tu, unapata wapi ujasiri wa kusikiliza mazungumzo ya mama na mwanawe?”

Shadia alishtuka, akihisi kama kauli hiyo ilikuwa kama kisu moyoni mwake. Alibaki kimya, macho yake yakatafuta msaada kwa Yasin, lakini hakupata maneno ya kujitetea.
“Mama, yeye si mfanyakazi. Yeye ni mgen...” Yasin alianza kusema, lakini kabla hajamaliza, Bi Leila alimkatiza.
“Nenda jikoni ukae na Sima. Nahitaji kuzungumza na kijana wangu,” alisema kwa
sauti ya amri, hata bila kumwangalia Shadia tena.
Shadia alisimama polepole, akihisi kutengwa na kudhalilika. Hata hivyo, alitii na kuelekea jikoni kimya kimya.

Bi Leila alipobaki na mwanawe, Yasin alimwelekea kwa uso wa wasiwasi.
“Mama, kuna nini kimetokea kuhusu mradi wako?” aliuliza kwa sauti ya huruma.
Bi Leila alikuna paji lake, akionekana kuchoka. “Ni mgahawa ule niliokuwa naufanyia ujenzi. Walikosea kazi kwenye kuta za ndani, na sasa kuna hitilafu kubwa. Nimepoteza muda na pesa kwa watu wasiowajibika!” alisema kwa hasira iliyopoa kidogo.
Yasin alimsikiliza kwa makini, kisha akasema, “Pole sana, Mama. Lakini najua utashughulikia hili vizuri. Mradi wako ni mzuri, na ni bahati mbaya tu umeangukia kwenye mikono ya mafundi wasio makini.”

Maneno yake yalionekana kumfariji Bi Leila kidogo, na akapumua kwa utulivu zaidi.
“Asante, mwanangu. Nitatatua hili, lakini inakera sana,” alisema, macho yake yakionyesha hasira iliyobakia kidogo.
Shadia akiwa jikoni, alisimama pembeni huku akishika glasi yake ya maji. Uso wake ulionyesha unyonge wa ndani. Kabla hajapata nafasi ya kuendelea kufikiri, Sima alimkaribia kwa tabasamu la upole, akisema, "Usijali, dada. Mama Leila siku zote ni mkali pindi tu Bwana Saleh anapokuwa hayupo. Huo ndio mwenendo wake, lakini utamzoea."
Maneno hayo yalionekana kama faraja ndogo kwa Shadia, lakini bado hakujisikia huru kabisa. Alishusha pumzi ndefu na kumtazama Sima

kwa macho ya uaminifu, kisha akasema kwa sauti ya upole, “Naomba niseme jambo, kama hutojali... Ningependa tuwe marafiki. Kwani tangu nizaliwe, sijawahi kuwa na rafiki yeyote wa karibu zaidi ya mama yangu.”
Sima alisita kidogo, akimwangalia Shadia kwa mshangao. Hata hivyo, alitabasamu kwa upole zaidi. “Marafiki? Mbona hilo ni jambo jema. Hakuna tatizo. Lakini... hujawahi kuwa na rafiki? Kwa nini hivyo?” aliuliza huku akichukua jagi
la maji na kulirejesha mahali pake.
Shadia akayumbisha kichwa chake kidogo, macho yake yakitazama chini. “Sina jibu sahihi...
Ila maisha yangu hayakuwa rahisi. Mama yangu alikuwa rafiki yangu wa pekee. Na kuhusu kazi za pamoja, sijui chochote, zaidi ya chache sana

za mimi kama mimi. Mama alifanya kunifundisha kila kitu kwa siri.”
Sima alimsikiliza kwa makini, kisha akasema kwa sauti ya utulivu, “Usijali, Shadia. Tutaelewana. Naweza kukufundisha chochote unachohitaji kujua. Hapa utajifunza polepole, na utaweza kujenga maisha yako mwenyewe. Niko hapa kwa ajili yako.”
Maneno hayo yaliufariji moyo wa Shadia, na akajikuta akitabasamu kwa mara ya kwanza siku hiyo. “Asante, Sima. Naahidi nitajitahidi,” alisema kwa sauti yenye tumaini.
Sima alimshika mkono kwa upole, ishara ya uaminifu mpya uliokuwa ukijengwa kati yao, na wote wawili walirejea katika kazi za jikoni,

Shadia alihisi kidogo kama amepata rafiki wa kweli.


Soma Kitabu

SOMA MAELEKEZO

Bonyeza hi "Soma Kitabu" kisha itakupeleka kwenye fomu yaku login, hakikisha ume login na namba uliyojiunga nayo ndipo utaendelea sasa kusoma kitabu chote