UMESHAWAH KUPENDA KWA KUONA MARA MOJA (wazungu wanaita love at first sight)
Embu tuambie, ukikutana na kijana au bint mrembo kwa mara ya kwanza utafanya Nini...
Maana hapa Kuna Yasir na yasin, vijana mapacha ambao wanakuja kumpenda bint shadia , ambae aligongwa na gari na baba yao baada ya shadia kutorooka kijijin kwao ambapo alikuwa anataka kuuliwa kwa sababu YEYE alikuwa ni pacha wa pili, na ukoo wao hautuhusu watoto mapacha, hivyo pacha ambae atazaliwa wapili anapaswa kuuwawa, ndicho kilichomkuta Shadia ila siku zake hazikuwa zimefika TU, mpaka alipoingia kwneye familia ya vijana wawili mapacha Yasir na yasin, wote wanaonekana kuvutiwa nae ila Yasir anapingana na moyo wake maana anajikuta kama hanaga muda na WAnawake na wakat NDUGU yake akijiaminisha kuwa moyo wake umeshamkubali bint shadia, anaetambulika kijijin kwao kama laana inayotembea, unadhan ni nani ambae atashinda vita hii ya mapenzi
SIMULIZI: SHADIA (LAANA
INAYOTEMBEA)
MTUNZI: SUMAIYA MWENDO
TUPOHAPA.COM
SEHEMU YA: 01
UTANGULIZI.........
Kijiji cha Warumi kilijulikana kwa utulivu wake, sheria kali za kimila, na maadili yaliyorithiwa kutoka kizazi hadi kizazi. Kijiji hicho kiliishi kwa kufuata mila na desturi zao kwa uangalifu mkubwa, na waliheshimu maamuzi ya viongozi wao, hasa Bwana Faki, kiongozi wa kijiji aliyependwa na kuheshimiwa na wengi. Lakini nyuma ya uso wa furaha na heshima, alibeba mzigo mkubwa moyoni mwke kutojaliwa kupata watoto kwa muda mrefu baada ya ndoa yake na Bi Maimuna.
Miaka kumi ilikuwa imepita tangu ndoa ya Bwana Faki na mke wake mpendwa Bi Maimuna, lakini hawakuwa wamebahatika kupata mtoto hata mmoja. Kila kona ya kijiji, watu waliongea kwa sauti za chini juu ya jambo hilo, wakidhani kuwa ilikuwa ni ishara mbaya kwa kiongozi wao, mtu aliyepaswa kuwa na uzao ili kuendeleza ukoo wake na kuhakikisha uongozi unadumu katika familia yake.
ENDELEA...........
"Wanandoa hao wamekaa miaka mingi bila mtoto," waliambiana wazee wa kijiji wakiwa wameketi chini ya mti mkubwa wa mwembe, "Labda mababu wamekasirika, au labda ni laana kwa Bi Maimuna. Haijawahi kutokea kiongozi wetu asiwe na watoto."
Lakini kwa upendo wake usio na mipaka kwa Bi Maimuna, Bwana Faki aliwatuliza wanakijiji kwa kusema waziwazi, "Sijali kuhusu maneno yanayosemwa kuhusu mimi kutopata mtoto, wala sitafanya maamuzi ya kutafuta mwanamke mwingine ili nizae, kwa sababu najua Mapenzi yangu kwaMaimuna ni makubwa, na zaidi ni kwamba naamini katika Mungu, najua kuwa wakati wa wetu ukifika tutapata tu. Mungu atatupa mtoto wakati anaopenda." Maneno hayo yalipooza mioyo ya wanakijiji kwa muda, lakini minong’ono iliendelea, hususan baada ya miaka mingi kupita bila kubadilika chochote.
Kila siku, Bwana Faki aliendelea kuonyesha upendo na kujitolea kwa mke wake. Aliamini kabisa kuwa mwanamke mwingine hawezi kujaza nafasi ya Bi Maimuna moyoni mwake.
Hakutaka ndoa nyingine kwa ajili ya kuridhisha jamii wala kujaribu kupata mtoto kupitia mwanamke mwingine. Na ndivyo ilivyoendelea, hadi siku moja, ilipotokea jambo ambalo lilibadilisha maisha yao kabisaa.
Asubuhi moja ya Jumapili, Bi Maimuna alimuita Bwana Faki kwa sauti iliyojaa furaha na mhemuko, "Mume wangu, nina habari njema!" Bwana Faki Alipokimbia kumfikia mke wake, alikuta machozi ya furaha yakitoka usoni mwa Bi Maimuna.
"Nina mimba!" aliongea kwa sauti yenye shauku na furaha, na kwa mara ya kwanza baada ya miaka kumi, Bwana Faki alihisi amani na furaha ambayo hakuwahi kuipata. Alimshika mke wake kwa mikono miwili na kumkumbatia kwa nguvu, akisema kwa sauti ya shukrani,
"Mungu ni mwema, amesikia sala zetu! Amejibu maombi yetu"
Wanandoa hao waliishi miezi tisa ya furaha, wakipanga jinsi watakavyomkaribisha mtoto wao wa kwanza na kuandaa sherehe kubwa kwa kijiji kizima. Bwana Faki alikuwa na furaha isiyokuwa na kifani; alihisi kuwa Mungu alikuwa amemjibu na kumbariki kwa sababu ya maombi yake ya siku nyingi na subra aliyokuwa nayo, na alienda msikitini kutoa swadaka kubwa kama ishara ya shukrani. Aliahidi mbele ya wanakijiji kuwa sherehe kubwa itafanywa pale mtoto wake atakapozaliwa, na wanakijiji walifurahia pamoja naye, wakisubiri kwa shauku kuzaliwa kwa mrithi wa ukoo wa Bwana Faki.
Hatimaye, siku ya kujifungua ilifika. Bi Maimuna aliharakishwa hospitalini, huku Bwana Faki akiwa amejaa tumaini na furaha ya kuona mtoto wake wa kwanza akija duniani. Alikaa kwenye kiti cha hospitali akisali kimya kimya, akihesabu dakika, na kila alipokumbuka ahadi ya Mungu kwake, moyo wake ulijaa matumaini.
Baada ya saa kadhaa za kusubiri, daktari alitoka na kumuita Bwana Faki. "Hongera, mke wako amejifungua salama," alisema kwa sauti ya utulivu. "Lakini kuna jambo moja unahitaji kujua. Amejifungua mapacha, mtoto wa kiume na wa kike."
Maneno hayo yalipomfikia akilini Bwna Faki, uso wa Bwana Faki ulibadilika ghafla. Furaha aliyokuwa nayo ilipotea kama upepo unaovuma
jangwani. Kwa kiongozi wa kijiji cha Warumi, mapacha yalikuwa ni jambo lisilokubalika. Katika familia yao, ilikuwa ni mwiko mkubwa, jambo lililozingatiwa kuwa laana kutoka kwa mababu zao wa kale.
Moyo wa Bwana Faki ulivurugika, akihisi msukosuko wa ndani uliomvaa. Machozi ya furaha ya muda mfupi tu uliopita yalibadilika kuwa ya hofu na masikitiko. Aliamini kuwa kujifungua mapacha kulimaanisha mikosi na mabalaa yatakayokumba familia yake na jamii nzima. Moyo wake ulipasuka vipande viwili— upande mmoja ukitaka kufurahia watoto wake, na mwingine ukihofia hasira za mababu na mila zao.
Aliingia ndani ya wodi, na alipoona mke wake akiwa na watoto wawili mikononi mwake,
alihisi maumivu na hasira kwa pamoja. Bi Maimuna alimkumbatia kwa upendo huku akimuonyesha watoto wao, macho yake yakiwa na mwanga wa furaha isiyokuwa na kifani. Lakini Bwana Faki hakuwa na utulivu tena; alisimama hapo, akitetemeka, akitafuta maneno ya kusema.
"Baba watoto," Bi Maimuna alisema kwa upendo, "tazama baraka ambazo Mungu ametupa." Lakini sauti ya Bwana Faki ilikuwa nzito na ngumu, "Unajua nini maana ya mapacha katika familia yetu? Huyu wa pili lazima aondoke katika dunia, la sivyo maafa yataanza kututembelea."
Bi Maimuna alihisi moyo wake
ukivunjikavunjika, lakini alikataa kwa ujasiri mkubwa hata kama alijua kila kitu. "Hawa ni
watoto wetu, na sitaruhusu hata mmoja wao kudhulumiwa. Kama ni laana, basi tutaishi nayo. Sitaki mtoto wangu afe!" Mpaka hapo Bwana Faki alihisi kama laana imeanza tayari..haikuwa imewahi kutokea hata mara moja mke wake akaacha kumtii
SOMA MAELEKEZO
Bonyeza hi "Soma Kitabu" kisha itakupeleka kwenye fomu yaku login, hakikisha ume login na namba uliyojiunga nayo ndipo utaendelea sasa kusoma kitabu chote