Penzi La Jini

book cover og

Utangulizi

Utangulizi
Katika ulimwengu ambapo binadamu na majini wanaishi kwa kufuata mipaka isiyoonekana, Sandra, binti wa kawaida mwenye ndoto kubwa, anakutana na Afrit Minal—jini mwenye nguvu isiyoelezeka, uzuri wa kuvutia, na siri nyingi za ulimwengu wa giza. Mkutano wao haukuwa wa bahati mbaya, bali hatima iliyoshonwa na nguvu zisizoeleweka.
Afrit, ambaye ameishi kwa zaidi ya miaka elfu kumi, anaingia katika maisha ya Sandra kwa njia isiyo ya kawaida, akivuruga kila kitu alichoamini kuhusu upendo, hatima, na maamuzi ya moyo wake. Licha ya tofauti zao, mvuto kati yao ni mkali, na mapenzi yao yanazama katika kina kisichozuilika—kiwango kinachoweza kubadilisha kila kitu, hata asili ya Afrit mwenyewe.
Katika hadithi hii ya mapenzi ya kusisimua na yasiyo ya kawaida, Sandra anajikuta akihamia ulimwengu wa starehe na maajabu, akiacha maisha ya kawaida nyuma na kuingia katika kifungo cha upendo kinachovuka mipaka ya binadamu na majini. Lakini je, mapenzi yao yanaweza kustahimili changamoto za dunia mbili tofauti? Je, Sandra yuko tayari kwa maisha yasiyo ya kawaida na mume asiye wa kawaida?
Karibu kwenye "penzi la jini", hadithi ya mapenzi, uchawi, na hatima isiyoepukika. 💫🔥

SEHEMU YA 1; SANDRA
Sandra alisimama mbele ya kioo chake cha zamani, akijitazama kwa macho yaliyojaa mawazo. Uso wake ulikuwa mzuri, lakini macho yake yalibeba uchovu wa ndoto alizokuwa akizisukuma kila siku. Alipapasa nywele zake laini zilizoshuka mabegani, akavuta pumzi ndefu kabla ya kubeba mkoba wake na kutoka nje.
Mji wa Chance Landing ulikuwa na pilikapilika za asubuhi. Mitaa yake ilijaa harufu ya kahawa kutoka kwenye vibanda vidogo, sauti za magari, na watu wakikimbizana na shughuli zao. Sandra alivuka barabara kwa haraka, akielekea Hobbes’ End, soko maarufu lililokuwa kitovu cha biashara za vito vya thamani. Ndani ya duka la Mpemba, ambapo alikuwa ameajiriwa, nuru ya almasi na dhahabu iling’aa kila kona, ikimkumbusha kwa mara nyingine kwamba alikuwa kwenye dunia ya matajiri, lakini yeye mwenyewe hakuwa mmoja wao.
Kila siku Sandra alipishana na wateja waliokuja na kutoka—wake wa matajiri, mabwana wa hadhi, na wasaka mali waliotaka kuwekeza kwenye vito vya thamani. Aliwahudumia kwa tabasamu, lakini ndani ya moyo wake kulikuwa na kiu ya kuwa upande wa pili wa biashara hii. Alijua kuwa hakuumbwa kuwa mtazamaji wa utajiri wa wengine, bali mmiliki wa dunia yake mwenyewe. Aliota siku moja atakuwa na nyumba kubwa, magari ya kifahari, na duka lake mwenyewe la vito. Ndoto hizi zilimfanya aamke kila siku na kujituma, lakini kila alipoongea nazo watu, walimcheka, wakiona kama anahangaika bure na kuota ndoto za Abunuwasi.
Mateo, mchumba wake, alizidi kuwa mgeni maishani mwake. Alikuwa tofauti sana na yule kijana aliyempenda mwanzoni—yule ambaye alikuwa akimtumia ujumbe kila asubuhi na kumfanya ajisikie malkia. Siku hizi, simu yake ilikuwa kimya. Hakumtumia tena maneno matamu, hakumtafuta kwa hamu kama hapo awali. Upendo wao ulikuwa baridi, na Sandra alihisi kama kivuli tu katika maisha ya Mateo. Alijaribu kujidanganya kuwa labda ni mawazo yake tu, lakini ukweli ulikuwa wazi—kuna kitu kilikuwa kimebadilika.
Usiku wa jana alijaribu kumweleza hisia zake, akamwambia wazi kuwa bado anampenda. Lakini Mateo alimkatisha kwa haraka, akimwambia kuwa alikuwa na watu wengi karibu naye na hawezi kusema chochote kwa wakati huo. Sandra alijikuta akiumizwa na majibu hayo, kwani mwanzoni haijalishi Mateo alikuwa wapi, hakusita kumwambia neno "nakupenda." Sasa, alihisi kama kivuli
tu katika maisha ya Mateo. Aliwaza, ni nini kilichobadilika? Kulikuwa na mwingine? Au labda yeye hakuwa wa kutosha tena?
Akiwa amezama kwenye mawazo, Sandra alishika mkufu mmoja wa almasi kwa uangalifu, akiuhamisha kutoka kwenye rafu hadi sehemu nyingine. Mwanga wa madini hayo ulirudisha ndoto zake kwa sekunde chache. Alijua siku moja angevaa vito vya thamani si kwa sababu ni sehemu ya kazi yake, bali kwa sababu ni sehemu ya maisha yake. Siku moja, angekuwa boss lady.
Lakini mpaka siku hiyo ifike, alikuwa hapa—akitafuta majibu katika maisha yaliyomzonga, akihisi upweke ndani ya mahusiano yaliyopoteza mwelekeo, na akihangaika kwenye ndoto ambazo wengi waliamini haziwezekani. Redio ikiwa inaimba mziki wa lana del rey ‘summertime sadness’, huku Sandra alichukua jukumu la kufanya usafi huku akijiimbia nyimbo kwa sauti ya chini ili kujiandaa kufungua ofisi yake na kuanza pilikapilika za siku hiyo.

SEHEMU YA 2; SANDRA
Siku ilikuwa imeanza vizuri kwa Sandra. Alikuwa kwenye kaunta, akipanga vito vya thamani kwa umakini, huku macho yake yakikagua kwa makini kuhakikisha kila kitu kipo mahali pake. Wateja walikuwa wakiingia na kutoka, wengine wakishangaa thamani ya vito hivyo, wengine wakinunua bila kuhoji bei.
Mara mlango wa duka ulifunguliwa kwa nguvu, na mwanaume mmoja aliyeonekana kuwa na hasira aliingia ndani. Alikuwa amevalia suti nadhifu lakini uso wake ulionyesha kutoridhika. Alitembea moja kwa moja hadi kwa Sandra na kuweka saa ya dhahabu mezani kwa kishindo.
"Nataka kurudisha hii saa!" alisema kwa sauti ya ukali.
Sandra aliinamisha macho yake na kutazama saa hiyo—ilikuwa bado mpya, iking'aa kama siku ilivyouzwa. Kwa utulivu, alimpigia mteja tabasamu la kibiashara na kusema kwa sauti ya upole, "Samahani sana mheshimiwa, lakini sera ya duka letu hairuhusu mteja kurudisha vito baada ya kununua. Tulikufahamisha hilo wakati wa manunuzi."
Mteja huyo alikunja uso kwa hasira na kuinua mkono wake kwa dharau. "Hivi unajiona wewe ni nani? Unajiona wa maana sana kwa sababu unafanya kazi
kwenye duka la vito? Wewe ni muuza duka tu, na utabaki kuwa muuza duka tu! Unajifanya unajua kila kitu, lakini huna maana yoyote kwenye maisha haya. Utazeea hapa ukiuza duka, na hutaendelea popote!"
Maneno hayo yalimchoma Sandra kama kisu. Alibaki mdomo wazi, macho yake yakianza kujaa machozi. Alijaribu kumeza hisia zake na kujifanya kuwa hayakumgusa, lakini moyoni mwake, alihisi kama mtu aliyepigwa na radi. Hakuelewa ni kwa nini mtu huyo alimvunjia heshima kiasi hicho. Ilikuwa haki gani mtu kumpuuza na kumdharau kiasi hicho?
Baada ya muda mfupi, mteja huyo aliondoka akibwatuka, akimwacha Sandra akiwa amesimama pale, akijaribu kuvuta pumzi na kujizuia kulia. Alihisi kuzidiwa na huzuni, lakini alijua hawezi kumruhusu mteja huyo kuona udhaifu wake. Alichofanya ni kuvuta pumzi na kuendelea na kazi, ingawa moyoni mwake kulikuwa na maumivu makali.
Aliporudi nyumbani jioni ile, maneno ya yule mteja yaliendelea kumrudia kichwani kama sauti ya dharau iliyoshindwa kufutika. Alijilaza kitandani, akiangalia dari kwa macho yaliyotota machozi. Alijiuliza, kweli maneno yale yalikuwa na ukweli? Je, alihukumiwa kubaki pale maisha yake yote? Hakika, hakuwa na maisha ya kifahari, lakini hakuwa na shaka kuwa siku moja mambo yangebadilika. Lakini, kwa nini maneno ya mtu asiyejua maisha yake yamuume kiasi hiki?
Kwa hasira na uchungu, alijikuta akitamani lau angerudisha muda nyuma, hata kufikiria kwa sekunde moja kwamba laiti angekuwa na bunduki, angempiga. Alitamani kuwa na maisha bora, maisha ambayo yasingemfanya adharaulike. Alihisi kama maneno ya yule mteja yaligusa kidonda chake cha ndani, sehemu ile yenye maumivu makali aliyokuwa akijaribu kuficha kila siku.
Lakini baadaye alifuta machozi yake na kuamua kuachana na mawazo hayo. Alijua hawezi kuwazuia watu kusema mambo juu yake, lakini pia alijua kwamba baadhi ya maneno yanauma sana. Aliamua kuyapuuza, lakini ndani kabisa ya moyo wake, alijua kuwa hangeweza kuyasahau haraka.
SEHEMU YA 3; Afrit
Katika ulimwengu wa majini, mbali na macho ya wanadamu, kulikuwa na mji wa kufikirika uitwao Bleakstone. Mji huu ulijaa viumbe wa ajabu, kila mmoja akiwa na nguvu za kipekee, lakini hakuna aliyemfikia Afrit Minal kwa uwezo. Alikuwa kiongozi wao, jini aliyeishi zaidi ya miaka elfu kumi, mwenye nguvu
zisizopimika na uzuri wa kuvutia mno. Alijua kuwa alikuwa mzuri, na kila kiumbe aliyekutana naye alikiri hilo. Lakini alisikitika jinsi wanadamu walivyodhani majini ni viumbe wa kutisha, wasiojua kuwa wanaishi nao kila siku bila hata kugundua.
Kwa muda mrefu, Afrit Minal alikuwa akitekeleza jukumu lake kubwa— kuteketeza madini adimu ya blue opal, madini pekee yaliyokuwa na uwezo wa kuwazuia majini kuingilia maisha ya wanadamu. Alijua kuwa mawe haya yalikuwa tishio kwao, na hakuwa tayari kuona nguvu za majini zikizuiwa. Hivyo, alizunguka katika kila duka la vito, akiwatumia wanadamu wenye tamaa kuyanunua madini haya na kuyateketeza, akihakikisha hakuna kilichosalia.
Siku moja, katika pitapita zake, alijikuta kwenye soko maarufu la Hobbes' End, mahali palipojaa vito vya thamani na wanadamu waliokuwa wakisaka utajiri. Aliingia kwenye duka moja lililojaa nuru ya almasi na dhahabu, akitazama kwa macho yake makali, akitafuta blue opal. Lakini kabla hajafanikiwa, macho yake yalivutwa na kitu kingine—mtu.
Binti mmoja alisimama nyuma ya kaunta, akihudumia wateja kwa sauti ya upole na tabasamu lililojificha nyuma ya huzuni nzito. Urembo wake haukuwa wa kawaida, ulikuwa wa kipekee kiasi kwamba hata jini mwenye umri wa milenia alishtushwa. Afrit Minal alisita kwa sekunde kadhaa, akishangaa jinsi mwanadamu anaweza kuwa na uzuri wa aina hii—na cha kushangaza zaidi, hakuwa na jini wa ulinzi. Kila binadamu mwenye sura ya kupendeza mara nyingi alikuwa na jini aliyemzunguka, lakini huyu hakuwa na hata chembe ya ulinzi wa kiroho. Hili lilimvutia zaidi.
Akiwa bado anamtazama, ghafla mlango wa duka ulifunguliwa kwa nguvu, na kijana mmoja akaingia akiwa na hasira. Bila hata salamu, alianza kumkalipia binti huyo kwa sauti ya ukali, akimlazimisha kusema jambo ambalo hakuwa tayari kulisema. Afrit Minal hakuhitaji kusikia maneno yao ili kujua kilichokuwa kinatokea—aliweza kuona nafsi ya binti huyo, jinsi maneno yale yalivyomuumiza, jinsi moyo wake ulivyokuwa ukivunjika vipande vidogo. Lakini cha kushangaza zaidi kilitokea sekunde chache baadaye.
Msichana huyo alipotazama chini kwa huzuni, machozi yakimlenga, Afrit Minal alihisi kitu cha ajabu kwenye nafsi yake—chozi likimdondoka. Kwa zaidi ya miaka elfu kumi, hakuwahi kulia. Hakuwahi kuhisi maumivu yanayotokana na huzuni ya binadamu. Lakini sasa, machozi yalikuwa yamemtoka kwa sababu ya
msichana huyu. Alisimama pale akiwa hajielewi, akihisi kitu ndani yake kikiwa kigeni na cha kutisha.
Hili lilimfanya kuchukua uamuzi wa haraka—angechunguza zaidi kuhusu yeye. Alitaka kujua kwa nini msichana huyu alikuwa tofauti. Kwa nini hakukuwa na jini wa kumlinda? Kwa nini urembo wake ulikuwa wa kuvutia kiasi cha kumgusa hata kiumbe wa ulimwengu mwingine? Na kwa nini, kwa mara ya kwanza katika maisha yake marefu, alikuwa amehisi?
Kwa mara ya kwanza, Afrit Minal alipata sababu ya kufuatilia binadamu mmoja, na hakuwa tayari kumuacha. Na ndipo akajua kuwa anaitwa Sandra n ani binti mwenye Maisha ya kawaida na mwenye ndoto kubwa saana za mafanikio lkn hakuna anaemuamini. Shauku ya kumjua Zaidi Sandra ikamuingia Afrit na akaamua kumfatilia Sandra mpaka wakati alipofunga na kuanza kurudi nyumbani kwake.
SEHEMUYA 04; Afrit
Afrit Minal alisimama juu ya dari la giza akimtazama Sandra kwa macho yasiyoonekana na binadamu wa kawaida. Alikuwa amemsindikiza binti huyo kutoka sokoni hadi nyumbani kwake bila yeye kujua. Lakini jambo lililomshangaza zaidi lilikuwa harufu ya nyumba ya Sandra—marashi laini yenye mvuto wa ajabu, marashi yaliyomfanya atamani kukaa humo milele.
Lakini hamu yake ya kubaki humo ilikatizwa ghafla na mabadiliko ya ghafla ya Sandra. Alimwona akitupa mkoba wake kwa hasira kando ya kitanda, akishika kichwa chake kwa maumivu ya ndani yasiyoelezeka. Kisha ghafla, machozi yalianza kumtiririka mashavuni mwake, akalia kwa uchungu na majonzi makubwa.
Kwa miaka elfu kumi aliyokuwepo duniani, Afrit Minal hakuwahi kushuhudia kitu kama hiki. Hisia zilimtanda—hisia ambazo hakuwahi kuzihisi hapo kabla. Kwa nini huzuni ya binti huyu inamuumiza hivi? Kwa nini hawezi kuvumilia kumuona Sandra akilia?
Alichotambua kwa haraka ni kwamba hakutaka tena kumuona Sandra katika hali hii ya huzuni. Lakini hakuwa na uwezo wa kumliwaza au kumfanya anyamaze. Hakuwa na njia ya kumfanya asihisi uchungu huu. Jambo pekee aliloweza kufanya ni kumtafuta aliyemsababisha mateso haya. Hivyo, bila kusita, aliamua kumtafuta mtu aliyemuumiza Sandra.
Kwa kutumia uwezo wake wa kipekee, aliingia katika ulimwengu wa ndoto na kumtafuta mteja aliyemvunjia Sandra heshima na kumdharau dukani. Aliyapata mawazo yake haraka, na bila huruma, akaingia ndani ya ndoto zake.
Katika ndoto hizo, Afrit Minal alijitokeza akiwa amejazwa ghadhabu na sauti nzito yenye mamlaka. “Sandra ni mali yangu! Hakuna mtu anayeweza kumuudhi na akabaki salama.”
Mteja huyo alitetemeka kwa hofu asijue kinachoendelea. Ghafla, ndoto yake iligeuka kuwa jinamizi la kutisha—hali ya giza lisilo na mwisho ilimzingira, sauti za watu waliokuwa wakilia kwa mateso zilijaa hewani, na kila kona alipogeuka aliona macho mekundu yakimwangalia kwa hasira.
Akazidiwa na woga. Moyo wake ukapiga kwa kasi, mapigo yake yakitishia kupasua kifua chake. Hali hii iliendelea hadi akili yake iliposhindwa kustahimili. Alishtuka kutoka usingizini akiwa na mawenge makali. Hakujua nini kilimtokea, lakini hakuweza kuhimili hofu aliyoihisi. Kwa mshtuko na hofu kali, alikimbilia nje ya nyumba yake, akihema kwa nguvu.
Alianza kukimbia bila mwelekeo, mwili wake ukiwa dhaifu na akili yake ikiwa imetetereka kabisa. Hakujua alikokuwa anakimbilia, lakini mguu wake ulimwongoza moja kwa moja hadi karibu na duka la Hobbes' End. Watu walimtazama kwa mshangao, wakijiuliza ni kwa nini kijana huyo anakimbia ovyo mitaani kama mtu aliyepagawa.
Ghafla, sauti kali ya honi ilisikika!
Dereva aliyekuwa mlevi alijaribu kusimama, lakini ilikuwa too late. Kijana huyo aligongwa vibaya na kutupwa mbali. Watu walipiga mayowe, wengine wakikimbilia kumsaidia, lakini tayari damu ilikuwa ikimwagika barabarani.
Afrit Minal, aliyekuwa akitazama kutoka mbali, alifunga macho yake kwa sekunde moja, kisha akafungua tena macho yake mekundu kwa maamuzi thabiti. Hakumuua kwa mikono yake, lakini alikuwa amemsababisha kufikia mwisho wake. Hilo lilitosha kwake.
Hakutaka tena kumuona Sandra akihuzunika, na kwa hilo, mtu aliyemletea mateso alikuwa amelipa gharama yake.
SEHEMU YA TANO
Sandra aliamka asubuhi na kurejea katika maisha yake ya kawaida. Alioga, akavaa nguo zake vizuri, kisha akapulizia marashi yake anayoyapenda. Kabla ya
kutoka, alimtumia Mateo ujumbe mfupi wa kumtakia siku njema kazini. Ilikuwa ni wajibu tu—hakukuwa na msisimko wala matarajio yoyote kutoka kwa Mateo. Alijua fika kuwa mapenzi yao yalikuwa yamefifia, na hata kama angejitahidi vipi kulihuisha, ilikuwa kazi bure.
Alipotoka nje, jua la asubuhi lilikuwa limetanda juu ya anga, na hewa ilikuwa tulivu. Alitembea kwa mwendo wake wa kawaida kuelekea kazini, akipita mitaa iliyojaa harakati za watu walioamka mapema kutafuta riziki. Alipokaribia soko maarufu la Hobbes' End, alikumbana na msongamano mkubwa wa watu. Kelele zilienea kila kona, watu wakinong’ona huku wengine wakijaribu kujua kilichotokea.
Akivutwa na udadisi, Sandra alijichomeka ndani ya umati, akijaribu kuona kilichowafanya watu wakusanyike kiasi hicho. Macho yake yaliangukia mwili wa kijana aliyelala katikati ya barabara, damu ikimtoka kwa wingi. Alikuwa amepoteza maisha papo hapo baada ya kugongwa na gari lililoondoka kwa kasi bila kusimama.
Damu ilimtia hofu, na hakuweza kuendelea kutazama. Alijitoa kwenye msongamano na kuelekea kazini kwake akiwa na mshtuko moyoni. Kifo kilikuwa kitu cha kutisha.
Alijaribu kujishughulisha na kazi zake ili kufuta taswira ya tukio hilo kichwani mwake. Hata hivyo, saa chache baadaye, alipokea wageni kutoka kituo cha polisi. Waliingia ndani ya duka lake kwa heshima, lakini sura zao zilionyesha kuwa walikuwa na maswali mazito.
"Tunaomba radhi kwa usumbufu, lakini tuko hapa kwa uchunguzi wa tukio la asubuhi," alisema mmoja wa maafisa hao.
"Tunaomba tuangalie CCTV kamera za duka lako, hasa zile za usiku wa kuamkia leo. Kulingana na ripoti za kamera za jirani, tunaamini gari lililomgonga marehemu lilitoka kwenye upande huu wa barabara, na dereva alikimbia."
Sandra aliwapeleka kwa CCTV bila kusita. Polisi walipoonyesha picha ya mwili wa marehemu, mwili wake ulisisimka ghafla.
Alitumbua macho kwa mshangao, pumzi yake ikawa nzito.
Hakuwa anahitaji kuthibitisha tena—alikuwa ni yule yule kijana aliyemtazama jana kwa hasira kali, yule aliyemfanya ajisikie vibaya mbele ya watu!
Lakini sasa… hakuwa tena duniani.
Baada ya polisi kuondoka na kuchukua nakala za CCTV, Sandra alijikuta bado ameshtuka na hana amani kabisa. Hisia zake zilichanganyika—alisikitika kwa kifo cha kijana yule, lakini pia alihisi woga wa ajabu. Ilikuwa ajali mbaya, lakini moyoni mwake kulikuwa na kitu kisichofahamika, kana kwamba kuna zaidi ya kile alichokiona kwa macho yake.
Aliamua kujitupa kwenye kazi ili kupotezea mawazo. Wateja waliingia dukani, wakiangalia vito vya thamani vilivyoonyeshwa kwa mwangaza mzuri wa madini yanayong’aa. Aliwahudumia kwa tabasamu la bandia, akijitahidi kutoonyesha msongo wa mawazo aliokuwa nao.
Majira ya mchana, mlango wa duka ulifunguliwa kwa upole, na bosi wake, Mpemba, aliingia. Alikuwa mzee wa makamo, mwenye mvi chache kichwani, akivaa suti ya gharama na saa ya dhahabu mkononi. Alimpenda Sandra kama binti yake na alimheshimu kwa bidii yake kazini.
“Sandra, binti yangu, habari za leo?” aliuliza kwa sauti yake tulivu lakini ya mamlaka.
"Mzuri bosi, karibu sana," Sandra alijibu kwa heshima, ingawa sauti yake haikuwa na nguvu kama kawaida.
Mpemba alimtazama kwa makini, akigundua kuwa alikuwa na kitu moyoni. “Ninajua kuna kitu kinakusumbua,” alisema huku akiweka mkoba wake mezani. “Nimekusikia asubuhi, kuna ajali ilitokea karibu hapa. Upo sawa kweli?”
Sandra alijaribu kutabasamu, lakini bosi wake alimfahamu sana. “Ni ajali tu, bosi. Lakini… sijisikii sawa. Nadhani ni mshtuko tu.”
Mpemba alitikisa kichwa kwa kuelewa, kisha akatoa funguo mfukoni na kuielekeza kwa ghala lililokuwa nyuma ya duka. “Nilikuja pia na bidhaa mpya leo, Sandra. Madini ya thamani sana.”
Alimwongoza Sandra kuelekea ghala, akafungua kabati kubwa lenye madini adimu kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Miongoni mwao, alifunua kisanduku kidogo kilichokuwa na mawe ya thamani ya bluu opal. Mara tu alipoondoa kifuniko, mwanga wa madini hayo ulijaa ndani ya chumba, ukirudisha mng’ao wa bluu safi.
Sandra alisahau msongo wake kwa sekunde chache na kutazama mawe yale kwa mshangao. “Haya ni mazuri sana, bosi! Yanatoka wapi?”
Mpemba alitabasamu. “Yametoka Afghanistan. Nilikuwa na dili kubwa kuyapata, na najua wateja watafurahia. Unajua kuwa madini haya yana thamani kubwa?”
Sandra alitikisa kichwa. “Ndiyo, huwa wanasema yana nguvu fulani ya kipekee.”
Mpemba alikiri hilo. “Wengi wanayaamini kwa mambo ya kiroho na ulinzi. Lakini sisi tunajali thamani yake kwenye soko.”
Alichokosa kujua ni kwamba nje ya duka, kivuli kisichoonekana cha Afrit Minal kilikuwa kimesimama, akishuhudia kila kitu kwa macho yake ya majini. Alipoona madini yale ya bluu opal, uso wake ulifunikwa na giza la hasira.
Haya ndiyo madini aliyoyatafuta kwa muda mrefu. Yale yale yanayoweza kumfukuza kutoka kwa maisha ya binadamu.
Na sasa… yako mikononi mwa Sandra.
SEHEMU YA 6; AFRIT
Usiku ulikuwa umetanda vizuri Sandra alipowasili nyumbani kwake baada ya siku ndefu kazini. Mwili wake ulikuwa umechoka, lakini akili yake ilikuwa bado imetawaliwa na matukio ya siku hiyo—ajali ile mbaya, mazungumzo yake na Mpemba, na yale madini ya bluu opal yenye kung'aa kupita kawaida.
Aliyapuuza mawazo hayo na kuelekea jikoni, akiamua kujipikia chakula chake alichokuwa akikitamani kwa muda mrefu—ndizi nyama. Harufu tamu ya mboga ilijaza nyumba yake ndogo, ikimfanya ahisi utulivu kwa mara ya kwanza tangu asubuhi. Alikula kwa utulivu, huku sauti ya redio yake ikicheza muziki wa ‘im yours- isabel LaRosa’ pole pole akitamani hata Maisha yake ya mapenzi yakngekaa sawa, maana alihisi hakuna kitu kinachoenda sawa kwake tena.
Baada ya chakula, aliosha vyombo na kisha kuelekea chumbani kwake. Alivaa nguo za kulalia kaptula fupi ya silk ilioonesha mashavu ya matako yake na topilioishia juu ya kitovu huku umbile lake lote likiwa nnje. Akijifunika shuka lake, macho yake yaliangaza juu ya dari, akiwa amezama kwenye tafakari nzito.
"Ndoto yangu ni kuwa boss lady, kuwa na nyumba yangu, magari yangu… lakini kuna jambo moja bado sijapata," alijisemea kimoyomoyo.
Alikuwa na kila sababu ya kuwa na furaha, lakini moyo wake ulikuwa mtupu. Upendo wa Mateo haukuwa tena kama ule wa mwanzo. Alitaka mtu wa
kumpenda kiasi cha kushindwa kupumua, mtu atakayemfanya ahisi thamani yake, sio kama vile Mateo alivyokuwa akimfanya ajihisi kama mzigo.
Alihema kwa uzito, kisha akageukia upande mmoja wa kitanda na kupitiwa na usingizi taratibu…
Ndani ya usingizi wake, Sandra alisikia jina lake likiitwa kwa sauti ya upole lakini yenye mamlaka. “Sandra…”
Bila hata kufikiria, alijikuta anaitika, "Abee?"
Kisha, akajikuta kwenye ndoto isiyo ya kawaida. Alikuwa ndani ya nyumba yake, lakini milango na madirisha yote yalikuwa wazi. Kulikuwa na mwanga hafifu wa kimya, na upepo mtulivu ukizunguka.
Alisikia mlango ukigongwa. Bila hofu, alisimama na kwenda kuufungua, akijua tu ni mgeni fulani aliyefika. Lakini alichokikuta kilimfanya ashtuke kidogo.
Mbele yake alisimama kijana mmoja mtanashati ajabu—mrefu, mwenye mwili wa kuvutia, ngozi yake ikiwa na mng’ao wa ajabu kama dhahabu ya jua lililotua. Nywele zake zilikuwa nyeusi zenye mawimbi laini, macho yake yakimetameta kwa rangi isiyoelezeka, kana kwamba ilikuwa mchanganyiko wa dhahabu na kahawia iliyochanganywa na giza la usiku.
Alikuwa ameshikilia shada la maua, yenye harufu ya kuvutia isiyo ya kawaida.
“Haya ni kwa ajili yako,” alisema kwa sauti yenye mvuto, akimkabidhi Sandra maua yale.
Sandra alichukua shada hilo huku tabasamu kubwa likimjia usoni. Kila kitu kilihisi kuwa cha kweli mno.
Kijana huyo alisogeza mkono wake mbele, akisubiri Sandra atoe wake. Bila kufikiria, Sandra alinyosha mkono wake naye akauchukua kwa upole, kisha akaupeleka kwenye midomo yake na kuubusu kwa heshima.
Mara moja, mwili mzima wa Sandra ulisisimka kwa mshtuko wa ajabu! Kila unywele mwilini mwake ulisimama, na hisia ngeni zikaenea moyoni mwake.
Ghafla, macho yake yalifunguka!
Aliamka kitandani kwa haraka, mapigo ya moyo wake yakiwa juu, mwili wake ukitetemeka kidogo. Kitu cha ajabu ni kwamba, alihisi msisimko ule bado upo ndani yake, kana kwamba mguso wa yule kijana haukuwa wa ndotoni pekee.
Aliinua mkono wake alioubusu ndotoni na kuunusa…
Harufu ya ajabu, yenye marashi mazito na ya kuvutia, ilikuwa imetanda kwenye ngozi yake. Hiyo siyo harufu ya losheni yake, wala marashi aliyopulizia kabla ya kulala.
Aliyumbayumba kidogo kitandani, akitazama chumbani mwake. Ndani ya giza la usiku, harufu nyepesi ya maua ya jasmin ilianza kujaza hewa, ikiambatana na utulivu wa ajabu.
“Ndoto ilikuwa ya kweli?” alijiuliza kwa mshangao.
Lakini alijituliza na kujaribu kupuuzia hisia hizo, akiamini labda ilikuwa ndoto tu ya kawaida. Alijifunika shuka na kurudi kulala… lakini usiku huo, hakuwa peke yake.
Katika kona ya chumba chake, kwenye kivuli cha usiku, macho mawili yenye mwanga hafifu yalimuangalia kwa utulivu.
Afrit Minal alikuwa ameingia rasmi kwenye maisha yake.


Soma Kitabu

SOMA MAELEKEZO

Bonyeza hi "Soma Kitabu" kisha itakupeleka kwenye fomu yaku login, hakikisha ume login na namba uliyojiunga nayo ndipo utaendelea sasa kusoma kitabu chote