NDOA YA BINT MREMBO MWENYE AKILI ZA KITOTO NA KIJANA MWENYE BUSARA NA HEKIMA
hatma ni fumbo kubwa sana, bint wa kufahari Maurine anapata ajali mbaya baada ya kitupwa ghorofani na kusababisha kukimbizwa hospital, alipofika hospital katika huduma za hapa na pale anafungwa bandage mwili wake mzima na kupelekea kutotambulika, katika hospital hio hio bwana zavian nae aliletwa akiwa amepata ajali, na ajali ilikuwa mbaya sana maana ilihusisha vifo na majerui mengi kidigo, kitu kilichosababisha wauguzi kuwa na harakati nyingi Sana, na kupelekea Maurine kuhamishwa hospital na kwakuwa alikuwa amefungwa na bandeji kila Kona ya mwili wake, hata qlipobadilishwa hospital hakutambulika amepelekwa hospital gani kitu kilichosababisha bwana maurine kupoteza familia yake, na anapokuja kupona anapoteza kumbukumbu na kuwa na akili kama mtoto mdogo wa miaka miwili, sasa harakati za maisha zinakuja kumkutanisha bwana zavian na Maurine, na WAKATI huo zavian anapewa shart la kuwa, ili awe mrithi wa mali za familia yake, ni lazima aoe, ndipo zavian anakutana na Maurine barabaran akiwa hakumbuki hata jina lake na kutaka kumuoa baada ya Maurine kumuomba barger, zavian anaamin kuwa ni kheri kuoa mwanamke asiekuwa na ufahamu MZURI Wala tamaa ya mali kuliko Hawa WAnawake wa mjini bila kujua kuwa Maurine n Binti wa kipekee kwa bwana Herse, professa mwenye mafanikio zaidi kwenye mji wa Madrid, unataka kujua ndoa ya Maurine mwenye akili za kitoto baada ya kupoteza kumbukumbu na zavian kijana mwenye busara ilikuwaje, usikose Kisa hichi Cha kusisimua Cha since we met
ANZA NAYO...
SIMULIZI: SINCE WE MEET
MTUNZI: SUMAIYA MWENDO
SEHEMU YA: 01
Uwanja wa ndege wa Madrid ulikuwa umejaa harakati za hapa na pale, ndege zikishuka na kupaa kila baada ya dakika. Moreen, binti mrembo mwenye asili mchanganyiko ya Tanzania na Hispania, alitoka katika lango la wageni, akivuta begi lake la kisasa na kutembea kwa madaha. Mvuto wake ulikuwa wa kipekee—ngozi yake laini yenye rangi ya chotara, nywele zake zilizojaa na kunawiri, na tabasamu lake la kirafiki lililovutia macho ya watu wengi.
Macho yake yalitua kwa baba yake, Bwana Hersi, aliyekuwa amesimama pembeni akiwa amevaa suti ya bei ghali na kuongozana na wasaidizi wake wawili. Bila kusita, Moreen alikimbia kwa furaha, akamkumbatia baba yake kwa nguvu, kana kwamba alikuwa msichana mdogo tena.
"Binti yangu, mrembo wa kifalme," Hersi alisema huku akimkumbatia kwa furaha. "Hatimaye, umerejea nyumbani!"
"Ahsante, baba," Moreen alijibu huku akitabasamu. "Naona leo umeamua kunifanyia surprise kubwa—umemtafuta msichana mdogo ambaye anaendana na umri wangu ili umuoe aje kuwa mama yangu mpya, siyo?"
Hersi alicheka kwa nguvu. "Haiwezekani, malkia wangu! Helen anakuzidi miaka saba ni mingi sana kumlinganusha na wewe. Hata hivyo ana hekima na uvumilivu wa kushughulika na baba yako mtata, so mchezo."
Moreen kidogo alitabasamu kwa hila na kujibu. "Hapo baba umejiongelea ukweli. Lazima awe mwanamke mwenye moyo wa chuma kumvumilia mtu kama wewe."
Wakati huo, Hersi alitoa simu yake na kusema, "Ngoja nimtumie Helen picha yako. Atapenda sana kukuona." Hersi alituma picha ya Moreen hapo hapo na picha ikamfikia mlengwa na kuonyesha tick mbili.
"Ah-ah, baba," Moreen alimwambia kwa haraka huku akimnyakua simu yake. "Huu siyo wakati sahihi wa mama yangu mpya kunijua. Hebu tusubiri tuonane uso kwa uso. Surprise ni tamu zaidi." Moreen aliifuta picha kwa wote.
Upande wa Helen aliona picha ya msichana mdogo na mrembo imeingia kwenye simu yake na imefutwa.
Hersi alitabasamu, akitikisa kichwa kwa kujiamini. "Hiyo ni kweli Princess, hata hivyo utampenda ukimuona. Helen ni mwanamke wa kipekee sana. Amejaa upendo na heshima. Sijawahi kuona mwanamke kama yeye, tangu kifo cha mama yako."
Moreen alicheka kimya kimya, lakini maneno ya baba yake yaliongeza hamu ya yeye kukutana na mwanamke huyo. Hersi alimuaga Moreen, akimuahidi kwamba baada ya kikao cha haraka huko ofisini, wataenda pamoja kwenye harusi. Kwa sababu siku hiyo ndo ilikuwa siku ya harusi ya Hersi na Helen.
"Usiondoke hotelini, Moreen," Hersi alisema huku akimkumbatia tena. "Nitakurudia hivi punde. Sitachelewa kurudi kwenye siku yangu ya furaha."
Moreen alikubali kwa unyenyekevu, lakini mara baada ya baba yake kuondoka, alishindwa kuvumilia. "Nasubiri masaa matano kufanya nini?" Alijiuliza kwa sauti. "Nimemletea zawadi, na najua ananipenda. Sioni sababu ya kumsubiri baba, mia natangulia zangu ye atanikuta"
Alinyoosha mkono, na msaidizi wake alimkabidhi mifuko mitatu ya zawadi zenye vito vya thamani. Alitabasamu kwa furaha, akasema kwa sauti ya kujiamini, "Nitam-surprise mama yangu mpya. Hii itakuwa siku ya kipekee sana kwake!"
Kwa upande wa Helen, furaha ya harusi iliharibika mara baada ya kupokea ujumbe kutoka kwa Hersi. Alifungua simu yake na kuona picha ya msichana mrembo aliyeonekana mdogo sana—Moreen. Wivu na hasira zilimjaa, na akili yake ikamtuma kwamba Moreen alikuwa mchepuko wa Hersi.
"Naamini hilo," Helen alisema huku macho yake yakitisha, "nitakapokutana na huyo msichana hakika sitamuacha salama." Alimpigia simu Hersi, wakati huo Hersi alikuwa kwenye gari anaelekea ofisini.
"Mpenzi " alionge Hersi baada ya kupokea"
" Mpenzi wako nani Hersi, yaani bila aibu unanitumia picha ya mchepuko wako unamaliza unaifuta kweli?" Hersi hakuelewa huyu Helen ana maanisha nini?.
" Helen nahisi kuna kitu hukielewi, unawezaje kuwaza hivyo?"
" Hersi sijui kama ntakuelewa hata utumie njia gani?" Helen alikata simu hapo hapo.
Marafiki zake walijaribu kumtuliza, lakini hasira ya Helen haikuweza kuzimwa. Simu yake iliita tena, Hersi alikuwa akipiga. "Acha ujinga huo, Helen," alisema kwa sauti ya upole lakini yenye msisitizo. "Kuna mambo mazuri yanakuja mbele yetu. Amini tu kula kitu ni salama kwa upandewangu na usipende kumhukumu vibaya bila maelezo."
Helen alikata simu ghafla, akabaki na wazo moja—lazima ajue ukweli kuhusu huyo msichana mpuuzi na akimjua hawezi kumuacha salama. Aliwaza hivyo Helen akiamini Moreen ni mchepuko wa Hersi.
Moreen, akiwa ndani ya gari la kifahari, alitabasamu kwa matumaini. Moyo wake ulikuwa na hamu kubwa sana ya kumuona Helen, amjue kisha aolewe baba yake na waanze maisha mapya kama familia. Lakini hakujua kabisa kwamba safari yake ya furaha ilikuwa inampeleka kwenye tukio la maumivu yasiyotarajiwa. Maana Helen alitafsiri kivyake
SIMULIZI: SINCE WE MEET
MTUNZI: SUMAIYA MWENDO
SEHEMU YA: 02
Safari ya kurejea Hispania ilikuwa na kila dalili ya furaha kwa familia ya Karama. Zavian, kijana pekee wa familia hiyo, alikuwa na kila sababu ya kutabasamu, wazazi wake walikuwa wamepanga kumkabidhi rasmi kampuni yao kubwa, KARAMA'S CONSTRUCTION SUPPLIES akiwa na miaka 25 tu. Licha ya umri wake mdogo, Zavian alikuwa na akili ya biashara iliyomfanya astahili urithi huo mkubwa.
Ndani ya ndege ya kifahari wakiwa kama familia, Zavian na wazazi wake walikuwa wakiufurahia muda wao wa pamoja—kipindi cha nadra mno kutokea katika maisha yao ya kazi nyingi. Walikaa kwenye viti vya daraja la kwanza, wakitaniana kama marafiki wa karibu sana.
"Kwanza, siamini kama likizo hii mmekuba kuitumia mkiwa pamoja ba mimi, mpo bize sana jamani, hatimaye tumeweza kukaa na kuzungumza kwa utulivu kama familia," Zavian alisema huku akiwatazama wazazi wake.
" Kila mtu kati yetu amefurahia hilo wakati huu Z, ujue ubize ukizidi sana mtu una sahau kama hata una mume, sasa naelewa kwa nini watu wakubwa wanaume huwa wanakuwa na vimada" alisema mama Zavian
" sio tu wanaume mama, hata. Wanawake siku hizi wanavimada ebu fikiria kuhusu wewe na baba, kwa muda wa miezi mitatu wewe uko Paris baba yupo Japan. Nafasi ya kuonana mara moja kwa miezi mitatu na hamuoni shida"
" sasa mbona unatuingilis vibaya sana na wewe!" Baba yake alimsema Z akatabasamu na kumjibu.
" Hapana baba mimi nasema tu, usikute huko kwenye maisha ya watu, labda mimi tayari nina ndugu zangu wa kimya na sijui, baba kuwa romantic kwa mama , kama huwezi nambie nikupe ujuzi" mama yake alicheka
Baba yake, Mulky Karama, alicheka kwa sauti kubwa. "Usijifanye mjuaji sana, Z. Mpaka sasa hujui hata kuwa romantic kwa mwanamke. Mapenzi yako ya kwanza tu yamefeli, si ndio? Mwanamke akakuwacha eti hujui kuonyesha upendo! Muda mwingi upo bize mpaka akajiona kama vile hastahili kwenye maisha yako, akachukua hamsini zake "
Zavian alitikisa kichwa kwa tabasamu la aibu. "Hiyo ni zamani, baba. Nitaweka juhudi zaidi kwenye mahusiano yangu yajayo. Hata hivyo watu hujifunza kutokana na makosa, siyo?"
Mama yake, Bi Sofia, aliingilia mazungumzo kwa utani mkali. "Z, usimsikilize baba yako. Huyo mwenyewe hajui lolote kuhusu mapenzi. Naamini hata miaka yote ya ndoa yetu, sijawahi kuhisi kuwa na mtu 'romantic.'"
Mulky alimkazia macho Sofia kwa jicho la kushangaa. "Hivi unamaanisha nini, Sofia? Hivi nikikumbusha valentine za miaka iliyopita, si mara nyingi ulikua unanililia kwa furaha kabisa ukisema nimezidi?"
Sofia alicheka, akamshika mkono na kumsogelea. "Unajua nini? valentine zako, zilikuwa kama za watoto wa shule" Sofia alicheka Mulky akajisikia vibaya Sofia akamkumbatia. "lakini bado nakupenda." Alimkumbatia na kumbusu kwa upendo.
Zavian alicheka kwa nguvu, akiwatazama wazazi wake waliokuwa wakionyesha mapenzi kwa njia ya kipekee mbele yake bila hata kujali. Alitoa simu yake haraka, akasema, "Lazima nichukue picha ya kumbukumbu bhana. Sio rahisi wazee wa umri wenu kuonekana romantic mkiwa live."
Alipiga picha kadhaa huku wazazi wake wakitabasamu. Lakini wakati huo huo, mshangao ulianza kujitokeza ndani ya ndege. Kelele kidogo kutoka kwenye injini zilianza kusikika, zikitokea upande wa kushoto wa ndege. Mara nyingine injini ilitoa kishindo kikali, na ndege yote ikaanza kutikisika.
“Mama, baba... oneni?” Zavian aliuliza huku akiinua macho kwa wasiwasi.
Kabla hata Sofia hajajibu, kelele za rubani zilisikika kwenye spika:
“Samahani kwa usumbufu. Tumepata hitilafu kwenye injini ya kushoto, lakini tunaidhibiti hali. Tafadhali tulieni.”
Mulky alijaribu kutabasamu ili kumtuliza mke wake. "Ni kawaida tu, Sofia. Marubani wanajua wanachofanya. Tuwe na imani"
Lakini Sofia hakuhisi usalama kabisa. Alimshika mkono Zavian kwa nguvu. "Z, chochote kitakachotokea, nataka ujue kwamba tunakupenda sana. Na Una uwezo wa kushinda changamoto yoyote ile kwa hiyo usitetereke."
Maneno yake yalionekana kuwa kama ya mwisho. Ghafla, ndege ilianza kupoteza mwelekeo kwa kasi kubwa. Vilio vya abiria vilianza kusikika. Zavian alishikilia mkanda wake kwa nguvu, akiwatazama wazazi wake ambao sasa walikuwa wakisali kimya.
Milango ya dharura ilianza kupasuka huku hewa ikivuma kwa nguvu. Rubani alisikika kwa mara nyingine, sauti yake ikiwa na taharuki.
“Tafadhali fungeni mikanda kwa nguvu! Tutatua kwa dharura!”
Ndege ilianza kuanguka kwa kasi, ikiyumba huku na kule. Zavian, akiwa amebanwa na mkanda, alishuhudia wazazi wake wakipeperushwa. Alijaribu kuwafikia lakini kila kitu kilikuwa haraka sana. Hatimaye, ndege ilipiga kishindo kikubwa ardhini, kila kitu kikazama gizani. Na hakuweza kuona kitu chochote wakati huo ni kama vile alipoteza uhai kwa muda.
ITAENDELEA..........
SIMULIZI: SINCE WE MEET
MTUNZI: SUMAIYA MWENDO
SPONSORED BY: TUPO HAPA. COM
SEHEMU YA: 03
Moreen alishuka kwenye teksi akiwa amejaa furaha na msisimko. Alikuwa amevaa vizuri, gauni lake la rangi ya bluu lilimkaa vyema sana, na nywele zake zilifungwa kwa mtindo wa kifahari. Alitembea kwa kujiamini, akikodoa macho yake huku na kule akitafuta mlango wa nyumba ya Helen, mama yake wa kambo mtarajiwa.
Huku akiwa bado hajaanza kubisha hodi, alizungumza kwa simu na baba yake, Hersi, akimweleza, “Baba, nimeshindwa kukusubiri. Nimefika tayari hapa nyumbani kwa mama Helen. Nilitaka kumfanyia surprise.”
Hersi alicheka kwa upole. “Sawa binti yangu. Nitampigia Helen simu, nimwambie ajiandae kukupokea.”
Moreen alitabasamu. “Asante baba. Nakupenda sana.”
Kisha akakata simu, akapumua kwa kina kabla ya kubisha hodi. Huku ndani, Helen alikuwa akifoka kwa hasira akizungumza na rafiki zake Edina na Roselyn.
“Unajua, picha ya yule mchepuko imefutwa WhatsApp kwa sababu ya kuiona. Lakini bado taswira ya huyu binti wa kichokozi haijatoka akilini mwangu. Ana ujasiri gani yaani hadi kuingilia ndoa yangu na Hersi?” Helen alisema kwa sauti ya ghadhabu.
Edina, aliyekuwa akitazama dirishani, alimshika Helen bega. “Angalia nje! Yule binti mwenyewe si ndo yule.”
Helen aligeuka kwa haraka na kutazama dirishani. Alimtazama Moreen kwa macho ya chuki. Aliona jinsi alivyo mrembo, mwenye tabasamu la upole na sura ya aibu. Hasira zilimshinda. Akaelekea mlangoni kwa hatua za haraka huku akiongozana na marafiki zake. Wakafungua mlango kwa kishindo.
Moreen, alipomuona Helen akitoka, alitabasamu kwa furaha. Alikimbia kumkumbatia kwa sababu alimtambua kutoka kwenye picha. “Miss Helen! Ni mimi Moreen. Nimefurahi kukuona.”
Lakini kabla hajafikia, kofi zito lilitua shavuni mwake. Alisimama kwa mshangao, akishika shavu lake huku macho yake yakiwa yamejaa maswali.
“Unathubutu vipi kuja hapa, wewe kahaba mdogo!” Helen alimwambia kwa sauti kali.
Moreen alishangaa na kumtazama Helen "Sijui unazungumzia nini—” Moreen alijaribu kusema, lakini kofi jingine likatua upande mwingine wa shavu lake. Akajikuta ametua chini kama mzigo.
“Unajifanya hujui? Unajua kabisa kuwa wewe ni mchepuko wa Hersi, na bado una ujasiri wa kuja hapa lengo lako ni kunidhalilisha?” Helen alifoka kwa sauti kubwa.
“Hapana! Hersi ni baba yangu!” Moreen alijaribu kueleza, lakini Helen hakumsikiliza.
Helen aligeuka na kuwaamuru rafiki zake. “Shughulikieni huyu kahaba. Mfunzeni adabu!”
Edina na Roselyn walimvamia Moreen na kumziba mdomo wake kwa nguvu. Walimpiga na kumsukuma sakafuni. Moreen alilia, akihangaika kujinasua huku akipiga kelele kwa nguvu. “Tafadhali! Hersi ni baba yangu! Mmenielewa vibaya!”
Lakini kilio chake hakikusikika. Helen alienda pembeni kupokea simu kutoka kwa Hersi, ambaye alikuwa akimwambia kwa sauti tulivu, “Helen, nataka umpokee binti yangu kwa upendo. Atakuwa wa kwanza kufika hapo kabla yangu.”
Helen alijibu kwa sauti ya mahaba, kwa sababu alikuwa na hamu kubwa sana ya kumjua binti wa Hersi. “Usijali mpenzi. Nitamhudumia vizuri.”
Baada ya simu kukatwa, Helen alirejea na kuendelea kumpiga Moreen, akimsema, “Sasa utafurahia! Kwa sababu unapenda wanaume sana, nitakufanya ufahamu jinsi maisha yanavyokuwa mabaya kwa wasaliti! Eti wewe ni binti yake Hersi, ungekuwa Binti yake Hersi angenitaarifu mapema kabla haujaja, ila kanambia atafika kabla ya yeye kufika na sio wewe uliefika kwanza." Moreen alihisi kupagawa na hawa wanawake.
Mlango wa geti ulifunguliwa, na wanaume wawili wenye miili mikubwa waliingia ndani. Sura zao zilitisha, na macho yao yalionyesha ukatili. Helen aliwatazama kwa tabasamu lenye chuki na macho ya hasira. “Huyu ndiye kazi yenu leo. Mfundisheni adabu ajue adhabu ya kuingilia ndoa za watu ilivyo mbaya.”
Moreen, akiwa amezidiwa, alikodoa macho kwa hofu kubwa. Alijaribu kusema kitu, lakini sauti yake haikutoka. Alihisi maisha yake yakiteketea huku machozi yakitiririka usoni mwake. Inamaana wanaume hao wanaenda kumbaka au? Moreen alijawa hofu na huzuni kwa wakati mmoja.
SIMULIZI: SINCE WE MEET
MTUNZI: SUMAIYA MWENDO
SPONSORED BY: TUPO HAPA. COM
SEHEMU YA: 04
Kabla wanaume wale hawajamgusa Edna alimgeukia Helen na kumwambia muda umeenda inabidi wafike ukumbini haraka, kwani wageni tayari wameshafika na muda si mrefu. Binti yake Hersi atawasili na Hersi atafika kwa ajili ya ndoa. Helen aliona hiyo ni kweli hivyo alisitisha zoezi la Moreen kubakwa, ikabidi waelekee ukumbini. Aliwaamuru wale vijana wawili wambebe Moreen ili waende nae huko ukumbini. Vijana hao walifanya hivyo.
Ukumbi ulikuwa umejaa shamrashamra, watu wakiwa wamevaa mavazi ya heshima wakipiga soga na kusherehekea siku kubwa ya Helen. Wazazi wa Helen walikuwa wakijivunia binti yao, waliendelea kuwaeleza wageni kuhusu ndoa inayokuja na jinsi familia yao ingeimarika zaidi kutokana na ndoa hiyo.
“Binti yetu ni mwenye bahati sana kwa familia hii,” alisema mama yake Helen kwa tabasamu. “Tunajivunia kumuoza kwa mwanaume mwenye pesa zake, mwenye heshima, na anayejua thamani ya familia.”
Wageni walicheka kwa furaha, wakiipongeza familia ya Helen kwa mafanikio hayo. Na kuanza kujikomba komba kwao “Kwa kweli mmebarikiwa. Ni wachache wanaopata nafasi kama hii,” mmoja wa wageni alisema huku akitikisa kichwa kwa kupendezwa na hilo.
Mara mlango wa ukumbi ulifunguliwa kwa kishindo. Helen aliingia, akiwa kaongozana na marafiki zake Edina na Roselyn, huku nyuma wakifuatiwa na wale wanaume wawili wenye sura za ukatili wakiwa wamembeba Moreen kama mzigo. Macho ya kila mtu yalielekea kwao.
Wakati huo, wazazi wa Helen walinyanyuka kutoka kwenye viti vyao. Baba yake Helen aliuliza kwa sauti ya kushangaa, “Binti yangu, huyu msichana ni nani, na mbona yuko katika hali mbaya hivi?”
Helen alisimama katikati ya ukumbi, akiinua mkono kuonyesha umati utulie. Akakuna koo lake na kuanza kuzungumza kwa sauti ya kujiamini. “Huyu kahaba mdogo mnaemuona hapa?” aliongea huku akimwangalia Moreen kwa dharau. “Huyu ni mchepuko wa Hersi. Anajifanya kuwa binti yake ili nimuonee huruma, lakini ukweli ni kwamba huyu binti hana heshima hata kidogo. Anataka kuvuruga ndoa yangu!”
Ukumbi wote ulizizima kwa minong’ono na sauti za mshangao. Mama yake Helen alishtuka na kushika mdomo wake kwa mshangao. “Unasema nini, Helen? Mchepuko wa Hersi? Huyu binti mdogo sana kwa mambo hayo!” alisema huku macho yake yakimtazama Moreen kwa dharau.
Moreen, akiwa amewekwa chini na wale wanaume wawili, alijikongoja kwa taabu. Alikuwa hoi, damu ikitiririka kwenye paji la uso wake, na mwili wake ukiwa na michubuko kila kona. Alijaribu kufungua mdomo kuzungumza, lakini sauti yake ilikuwa dhaifu sana kusikika.
“Miss Helen, tafadhali… umekosea… mimi ni binti wa Hersi, Niamini.” aliongea kwa shida, machozi yakitiririka mashavuni mwake.
“Haa! Unathubutu kusema uongo mbele ya wageni wangu tena?” Helen alifoka, huku akipiga hatua karibu na Moreen na kumwangalia kwa hasira.
Mama yake Helen alisimama kwa hasira na kusema, “Kahaba mdogo kama huyu anastahili adhabu!” Kisha akachukua glasi iliyojaa kinywaji na kuitupa kwa nguvu kwenye uso wa Moreen.
Ndugu wengine walimfuata mama huyo, wakiwa na hasira, wakamrukia Moreen na kuanza kumvuta nywele zake huku wakimpiga kwa mateke na makofi. Wengine walirusha glasi na vitu vingine vilivyokuwa mezani, wakimlenga Moreen.
Moreen aliugulia maumivu, machozi yakitiririka kama mto. . Alijiuliza moyoni, “Ni vipi baba aliweza kuangukia kwenye penzi la mwanamke wa aina hii, na familia yenye roho mbaya kama hii?”
Wakati huo, Helen alikuwa akicheka kwa dharau, akifurahia kilichokuwa kinaendelea. “Haya ndiyo unayostahili kwa kujaribu kuingilia ndoa yangu!” alisema kwa sauti kubwa, akiwahimiza wengine waendelee na kile walichokuwa wakifanya.
Katika hali ya maumivu makali, Moreen alifumba macho, akihisi nguvu zikimwishia taratibu. Akiwa katikati ya umati wenye hasira, aliwaza kwa uchungu jinsi baba yake Hersi alivyompenda na jinsi upendo huo ulivyogeuka kuwa mateso makali kutokana na chuki za watu waliofungwa na dhana potofu. “Hivi nitapona katika mkasa huu?” aliwaza kabla ya giza kumvaa. Na bangili yake aliyoipenda kupindukia ikaanguka chini na kupasuka vipande vipande. Moreen alipoteza fahamu
Ukumbi ulitulia ghafla baada ya sauti ya heshima ya msaidizi wa Hersi kusikika mlangoni, “Bwana Hersi amewasili!” Kila mtu ndani ya ukumbi alishtuka, na hali ya wasiwasi ilitanda. Helen aligeuka kwa haraka, uso wake ukijawa na hofu iliyofichwa nyuma ya tabasamu la bandia.
SIMULIZI: SINCE WE MEET
MTUNZI: SUMAIYA MWENDO
SPONSORED BY: TUPO HAPA. COM
SEHEMU YA: 05
Ukumbi ulitulia ghafla baada ya sauti ya heshima ya msaidizi wa Hersi kusikika mlangoni, “Bwana Hersi amewasili!” Kila mtu ndani ya ukumbi alishtuka, na hali ya wasiwasi ilitanda. Helen aligeuka kwa haraka, uso wake ukijawa na hofu iliyofichwa nyuma ya tabasamu la bandia.
“Haraka!” Helen aliwaamuru wasaidizi wake kwa sauti ya chini lakini yenye mamlaka. “Mtoe huyo msichana hapa! Haraka, na hakikisheni hakuna dalili zozote za kile kilichotokea!”
Wanaume waliokuwa wamemtesa Moreen walimsogeza kwa haraka, walimbeba kana kwamba ni mzigo usio na thamani, na kumtoa kupitia mlango wa dharura ulioelekea sehemu ya nyuma ya jengo. Mfanyakazi mmoja alichukua kitambaa na kuanza kufuta damu iliyokuwa imeacha alama sakafuni, huku wengine wakihakikisha kila kitu kinarejea katika hali ya kawaida.
Helen alisimama katikati ya ukumbi, akihema kwa wasiwasi, akili yake ikijaribu kuunganisha kile kilichokuwa kinaendelea. Hersi alikuwa amesema binti yake angefika kwanza, lakini mbona sasa amewasili mwenyewe kabla yake? Swali hilo lilimfanya apate baridi ghafla, huku jasho likianza kumtoka kwenye paji la uso. Au Moreen huyu ndo binti wa Hersi? Alijiiza ila hakuamini moja kwa moja.
“Lazima niwe mwangalifu,” Helen alijisemea kimoyomoyo, akijaribu kutulia.
Mlango wa ukumbi ulifunguliwa, na Bwana Hersi akaingia akitabasamu. Alionekana mwenye furaha, macho yake yakitafuta haraka sura ya binti yake aliyekuwa amemsubiri kwa shauku kubwa. Alitegemea kumuona Moreen akikimbia kwa furaha na kumkumbatia kama kawaida yake, kwa sababu alifika kabla yake lakini hali ilikuwa tofauti.
Helen alijikakamua na kusogea mbele kwa haraka, akijifanya mwenye furaha isiyo na kifani. Alimkumbatia Hersi kwa nguvu, akisema kwa sauti tamu, “Mpenzi, pole na uchovu wa kazi. Najua safari ilikuwa ndefu hadi kufika hapa.”
Hersi alitabasamu kwa muda mfupi, lakini sura yake ilibadilika ghafla kuwa ya wasiwasi. Alimwangalia Helen kwa macho ya kuuliza, akisema kwa sauti ya utulivu lakini yenye mshangao, “Helen, nilisema binti yangu angefika kwanza. Yuko wapi Moreen?”
Helen alihisi moyo wake ukisimama kwa sekunde kadhaa. Alijaribu kudhibiti hali hiyo, na alijibu kwa tabasamu , “Oh, binti yako? Hata mimi namsuburi. Nadhani atakuwa karibu kufika hapa, usijali mpenzi.”
Hersi alimtazama Helen kwa jicho la shaka, lakini akaamua kutoendelea na mazungumzo hayo mbele ya watu wengi. “Naam, nitarajie kumuona hivi karibuni,” alisema kwa sauti ya upole. Kisha akatazama ukumbi mzima, akionekana kuchunguza kila kona.
Helen, akiwa bado katika hali ya taharuki, alijaribu kumshawishi Hersi asiwe na wasiwasi. “Mpenzi, twende tuketi. Wageni wengi wamefurahi kukuona, na chakula kiko tayari kila mtu yupo hapa kwa ajili yetu.”
Lakini Hersi hakujibu mara moja. Alisimama pale katikati ya ukumbi, akihisi kama kuna kitu hakiko sawa. Macho yake yalidumu juu ya eneo moja sakafuni, ambapo bado kulikuwa na alama hafifu za damu ambazo hazikufutika vizuri.
“Hii ni nini hapa?” aliuliza kwa sauti ya mamlaka, huku akiinama kuchunguza kwa makini.
Helen aliharakisha mbele, akijifanya hajui chochote. “Ah, ni sakafu tu. Labda ni madoa ya kawaida, wahudumu watashughulikia,” alisema kwa sauti ya kutabasamu lakini yenye hofu iliyofichika. Hakutaka kumpa Hersi wasiwasi ya aina yoyote ile.
Hersi hakusema kitu tena, lakini shauku yake ya kumuona Moreen iliongezeka zaidi. Alisimama wima, macho yake yakijazwa na mashaka makubwa. "Binti yangu yuko wapi, Helen?" alirudia tena kwa sauti nzito, akionyesha dalili za kutokuwa na subira.
☆☆☆☆☆
Hersi aliendelea kutazama ukumbi kwa macho makavu, sura yake ikijawa na mchanganyiko wa mshangao na hasira. Alimgeukia Helen, akafoka kwa sauti nzito:
"Helen, binti yangu yuko wapi?!"
Helen, ambaye tayari alikuwa ameshtuka, alirudi hatua kadhaa nyuma, akitetemeka kwa hofu. Alijaribu kujibu kwa sauti dhaifu, lakini maneno yalikuwa magumu kutoka. "M-Mpenzi... sijui... U-u-ulisema atafika kabla yako, lakini hajafika hadi sasa."
Hersi alizidi kuhamaki. "Nilizungumza na Moreen kabla ya kuja hapa! Alikuwa tayari yupo kwenye mitaa yenu. Ina maana alikuwa amefika hapa! Unataka kuniambia nini, Helen?"
Jina "Moreen" lilipozungumzwa kwa nguvu, ukumbi mzima ulijawa na mshangao. Wale waliomshambulia msichana aliyeletwa kwa dharau walikumbushwa kile walichofanya muda mfupi uliopita. Walitazamana kwa hofu kubwa.
Helen, sasa akiwa ametetemeka zaidi, alihisi miguu yake ikilegea. Alianguka kwenye kiti kilichokuwa karibu, uso wake ukiwa mweupe kama karatasi. “Moreen?” aliuliza kwa sauti dhaifu, kana kwamba hakutaka kuthibitisha ukweli huo.
Hersi alisogea mbele, macho yake yakitua kwenye kitu kilichokuwa sakafuni. Aliona kipande cha bangili ndogo iliyokuwa imevunjika. Alikiokota kwa mikono yenye kutetemeka, akakishika kwa nguvu huku akikumbuka vizuri. “Hii ni bangili ya Moreen,” alisema kwa sauti nzito iliyojaa uchungu. “Ina maana Moreen alikuwa hapa?”
Helen alijaribu kuinuka lakini hakuweza, hofu ilimlemea kabisa. Hersi alimsogelea kwa haraka, uso wake ukiwa umejawa na ghadhabu. Aliinama karibu naye, akamshika mkono wake kwa nguvu na kumuuliza kwa sauti iliyobubujika hasira:
"Niambie ukweli, Helen! Alikuwa hapa! Kimetokea nini?!"
Helen alitetemeka na kujaribu kujitetea. "N-nilidhani... nilidhani ni mchepuko wako! S-sikujua kama ni binti yako... nilidhani—"
Maneno yake yalikatishwa na kelele ya Hersi, "Nilidhani?! Nilidhani?! Huyo ni binti yangu, Helen! Ulimfanyia nini?!"
Helen alijaribu kuongea, lakini kabla hajamaliza, Hersi alimpiga kofi zito la mdomo lililosikika ukumbi mzima. Watu walitazama kwa mshangao, wengine wakaanza kunong’ona. Helen alishika shavu lake, machozi yakimtiririka.
"Kwa nini usiniamini?" Hersi alifoka, akijaribu kudhibiti hasira zake. “Kwa nini unafikiria ninaweza kutoka kimapenzi na msichana mwenye umri wa binti yangu?!”
Helen alibaki kimya, hofu ikizidi kuenea usoni mwake. Alifahamu kwamba alikuwa amekosea, na hakukuwa na nafasi ya kujitetea.
"Niambie, binti yangu yuko wapi sasa hivi?" Hersi aliuliza tena, akitembea kwa hasira huku akiikandamiza bangili ya Moreen mikononi mwake.
Kwa sauti dhaifu na yenye majuto, Helen alijibu, "Niliwaambia wale vijana wamtoe hapa na kumweka mahali pa usalama..."
Hersi alisikia hayo na hakusubiri maelezo zaidi. Aliwapigia kelele wale vijana waliokuwa sehemu ya tukio. “Nendeni mkamlete binti yangu sasa hivi! Ikiwa amepata madhara yoyote, nitahakikisha mnalipa!”
Wale vijana walikimbia nje ya ukumbi kwa haraka, wakiongozwa na hofu ya kile kingeweza kutokea. Lakini walipofika mahali walipokuwa wamempeleka Moreen, walishangaa kukuta eneo hilo likiwa tupu. Hawakumuona Moreen popote.
Walirudi haraka wakiwa wamejawa na wasiwasi, nyuso zao zikionyesha hofu kubwa. "Bwana Hersi," mmoja wao aliongea kwa sauti ya chini. “Tulimuacha hapo, lakini sasa hayupo. Hatuelewi alipoenda.”
Kauli hiyo ilimfanya Hersi apoteze subira kabisa. Aliwafuata moja kwa moja hadi mahali hapo. Alipofika, alisimama katikati ya eneo hilo, akitazama huku na kule. Hakukuwa na dalili zozote za Moreen.
“Binti yangu yuko wapi?!” Hersi alifoka kwa nguvu, sauti yake ikivuma kwenye anga la eneo hilo. Machozi ya hasira yalijikusanya kwenye kona za macho yake. Helen alikuja nyuma yake, akitetemeka, lakini hakuwa na jibu lolote la maana.
Hersi alimgeukia Helen kwa mara nyingine, akimuuliza kwa hasira kali, “Helen! Moreen yuko wapi?!”
Helen alitetemeka zaidi, akishindwa kabisa kusema neno lolote. Alijua ukweli mmoja tu—kilichotokea kingemgharimu kila kitu.
SIMULIZI: SINCE WE MEET
MTUNZI: SUMAIYA MWENDO
SPONSORED BY: TUPO HAPA. COM
SEHEMU YA: 06
Hersi alisimama katikati ya ukumbi, uso wake ukionyesha wazi mshangao na ghadhabu. Aliwavuta wageni wote macho kwa tamko lake zito. "Zoezi la ndoa hii limesitishwa rasmi kuanzia sasa," alisema kwa sauti kali iliyotulia ukumbi wote. "Mpaka binti yangu, Moreen, atakapopatikana salama."
Helen aliyekuwa bado akitetemeka, machozi yakitiririka mashavuni mwake, alijaribu kumwita Hersi, "Mpenzi..." lakini Hersi alimkatiza kwa mkono, ishara ya kutaka ukimya.
"Helen," Hersi alianza, sauti yake ikiwa ya chini lakini ikibubujika na hasira. "Nilikuamini. Nilikuona kuwa mwanamke wa heshima, nikakupa nafasi ya kuwa sehemu ya maisha yangu. Nilipanga kukuheshimisha, kukufanya mke wangu wa heshima. Lakini sasa..." Alimtazama Helen kwa macho makavu. "Nimeiona rangi yako halisi. Wewe na mimi hatuwezi kuwa kitu kimoja tena. Kwa sasa namtaka binti yangu. Na ikitokea hajapatikana, wewe na familia yako mtalipa gharama."
Maneno hayo yalimchoma Helen kama kisu moyoni. Alijaribu kusimama lakini miguu yake ilishindwa kuubeba mwili wake. Alianguka kwenye kiti, akikumbatia uso wake kwa mikono huku akilia kwa uchungu.
Ndugu zake Helen, waliokuwa wametulia nyuma ya ukumbi, walibadilika na kuwa na wasiwasi mkubwa. Walihisi hali ya hatari ikiwazunguka. Baba yake Helen, uso wake ulijaa hofu, alikumbuka kwa mshtuko tukio lililotokea awali.
Baba Helen alijikuta akikumbuka jambo.
Akiwa ameshikwa na hasira kali kwa dhana kwamba Moreen alikuwa mchepuko wa Hersi, baba yake Helen alijikuta akimpiga msichana huyo kichwani kwa chupa. Kupigwa huko kulimfanya Moreen kupoteza fahamu. Wakiwa hawajui cha kufanya, waliamua kumficha kwa siri nyuma ya ukumbi, wakitegemea kwamba hali hiyo itatatuliwa baadaye.
Kumbukumbu ya Kaka yake Helen
Kaka mmoja wa Helen, aliyekuwa amechukizwa sana na wazo la Moreen kuwa chanzo cha maumivu ya mdogo wake, alienda mbali zaidi ya hapo. Alipogundua kuwa wale vijana waliokuwa wamemficha Moreen waliondoka kwa muda, alienda na kumtoa Moreen kwa nguvu kwenye maficho. Kwa hasira kali, alimchukua hadi kwenye ghorofa ya juu ya ukumbi na kumtupa chini akisema kwa sauti kali:
"Mtu yeyote anayethubutu kuiharibu furaha ya Helen, matokeo yake ni kifo."
Moreen alitupwa kwa nguvu, mwili wake ukiporomoka hadi chini. Kumbukumbu yake ya tukio hilo iliishia hapo akabaki na hofu tupu.
Hersi, akiwa bado amepandwa na hasira, alirudi ukumbini. Alipofika, alikuta kundi la maafisa wa polisi wakiwa wameingia. Alisogea kwa kasi, macho yake yakitafuta majibu. "Nini kinaendelea hapa?" aliuliza kwa ukali.
Afisa mmoja alijitokeza mbele na kusema kwa sauti ya heshima, "Tulipokea taarifa kwamba kuna binti ameanguka kutoka ghorofa ya juu ya ukumbi huu. Hali yake ni mbaya sana. Hatujui kama alijirusha au alirushwa, lakini tuko hapa kuchunguza."
Hersi alishtuka, mapigo ya moyo wake yakipanda. "Binti huyo ni wa aina gani?" aliuliza kwa sauti iliyojaa wasiwasi.
Afisa huyo alieleza maelezo ya msichana huyo, akijaribu kuwa makini na maneno yake. Hersi alitetemeka, macho yake yakijaa machozi. "Huyo ni Moreen... binti yangu. Moreen hawezi kujiua. Bila shaka kuna mtu amemfanyia hivyo!"
Hersi aliongeza kwa haraka, "Yuko wapi sasa? Nipeleke kwake!"
Afisa alimweleza kuwa Moreen alikuwa amepelekwa hospitalini, lakini hali yake ilikuwa mbaya sana. "Hatujui kama ataweza kupona," alisema kwa tahadhari.
Hersi hakutaka kusikia maelezo zaidi. Alihamaki na kuelekea mlangoni, akijiandaa kwenda hospitalini. Lakini kabla ya kutoka, alimgeukia afisa huyo na kusema kwa sauti yenye mamlaka:
"Mkamate Helen na familia yake yote. Wote wanahusika na hili. Sitaki kuona hata mmoja wao akiondoka hapa kabla ya uchunguzi wa polisi kukamilika."
Helen alipigwa na butwaa, macho yake yakiwa mekundu kwa machozi. "Hersi... hunipendi tena? Hata kidogo?" aliuliza kwa sauti dhaifu.
Hersi hakutazama nyuma. "Nilikuwa nakupenda, Helen. Lakini ulichokifanya kimenionyesha ukweli wako. Furaha yangu pekee sasa ni kumpata binti yangu."
Helen alianguka chini, akilia kwa uchungu. Ndoto zake zote zilikuwa zimeyeyuka kama barafu kwenye jua kali. Kile alichodhani kingekuwa cha milele, sasa kimegeuka kuwa ni haitokaa itokee.
ITAENDELEA.........
[06/02, 15:42] Summy: SIMULIZI: SINCE WE MEET
MTUNZI: SUMAIYA MWENDO
SPONSORED BY: TUPO HAPA. COM
SEHEMU YA: 07
Hospitali ya Rufaa Ramón y Cajal, moja ya hospitali kubwa zaidi mjini Madrid, ilikuwa imefurika. Korido zilijaa wauguzi wakikimbia huku na huko, madaktari wakitoa maelekezo, na watu waliokuwa wakihangaika kujua hali za wapendwa wao. Miongoni mwao, Hersi aliingia, uso wake ukiwa umejaa huzuni na hofu isiyoelezeka. Alikuwa ameongozana na walinzi wake wawili, kila mmoja akijaribu kufungua njia kwenye msongamano wa watu.
Hersi alisimama katikati ya lango kuu, macho yake yakikagua hali ilivyo. Kulikuwa na makelele ya vilio vya watu waliopoteza wapendwa wao, wengine wakiomba msaada wa haraka kwa wauguzi. Hersi alijaribu kuvumilia hali hiyo, lakini moyo wake ulikuwa unamuuma mno. Alimgeukia mmoja wa walinzi wake na kusema kwa sauti ya amri:
"Nenda utafute mtu yeyote hapa anayeweza kutupa taarifa. Ninahitaji kujua hali ya binti yangu."
Mlinzi huyo alisogea kwa watu waliokuwa wamekusanyika pembeni ya korido na kuuliza nini kinachoendelea. Mtu mmoja, ambaye alionekana kama muhanga wa watu waliopata ajali ya ndege, alijibu kwa sauti ya huzuni, "Ndege moja iliyokuwa ikitoka Marekani imepata ajali ilipokuwa ikikaribia kutua. Wengi wa waliokuwemo wameumia vibaya, na baadhi yao wamefariki dunia. Hospitali hii sasa inashughulikia majeruhi wengi waliotolewa kwenye eneo la tukio."
Mlinzi alirudi haraka na kumwambia Hersi, "Mheshimiwa, ndege moja imeanguka karibu na uwanja wa ndege wa Madrid. Ndiyo sababu ya hali hii."
Hersi alishangaa, lakini taarifa hizo hazikumgusa sana. Alikuwa amezama katika fikra za binti yake, Moreen. Alitoa simu yake mfukoni na kuangalia taarifa za ajali hiyo. Aliona picha za ndege iliyokuwa imeharibika vibaya, miili ya watu ikitolewa, na majeruhi wakiwa wamebebwa kwenye machela.
Alisonya na kusema kwa sauti ya huzuni, "Mungu wangu, rehema zako zitawale kwa watu hawa... lakini sasa nataka kujua Moreen yuko wapi."
**Wodi ya Mahututi**
Wakati huo, katika moja ya wodi za watu mahututi, Moreen alikuwa amelazwa kitandani, mwili wake ukiwa umefungwa bandeji kila kona. Kichwa chake kilikuwa kimefunikwa na bandeji kubwa, damu zikiwa bado zinaonekana kwenye pamba zilizowekwa pembeni ya kitanda. Pembeni yake, kulikuwa na kitanda kingine ambacho alilazwa kijana mmoja mwenye nywele za kahawia na ngozi yenye mchanganyiko wa rangi za Kihispania na Kiafrika. Alikuwa Zavian, majeruhi wa ajali ya ndege.
Madaktari wawili walikuwa wakipitia ripoti za matibabu ya wagonjwa hawa wawili. Walijadiliana kwa sauti ya chini:
"Moreen amepata majeraha makubwa kichwani. Tunaweza tu kumuweka chini ya uangalizi wa karibu. Tutafanya CT scan mara nyingine leo jioni."
"Na huyu kijana, Zavian?" aliuliza daktari mwingine.
"Ameumia vibaya mgongoni. Tumeanza matibabu ya dharura, lakini hali yake bado ni tete."
****
Hersi alipofika mapokezi, alikuta mlango wa kuingia katika wodi ya mahututi umefungwa. Kulikuwa na walinzi waliokuwa wakizuia watu kuingia isipokuwa wagonjwa pekee. Alijaribu kuelezea hali yake, lakini walinzi hao walikuwa wakifuata maagizo ya hospitali.
"Nahitaji kuingia! Binti yangu yuko ndani ya wodi hiyo bila shaka, alipata ajali alianguka ghorofani," alisema Hersi kwa msisitizo.
Afisa mmoja wa hospitali alimkaribia na kusema kwa heshima, "Pole sana, mheshimiwa. Tunafahamu hali yako, lakini kwa sasa, wodi ya watu mahututi imejaa wagonjwa wengi. Tunaomba usubiri mpaka madaktari wakutaarifu."
Hersi aliguna kwa hasira. "Ninahitaji kumwona binti yangu. Sitaki kusikia kingine chochote."
Afisa huyo aliendelea kumtuliza. "Tafadhali, tunafanya kila tuwezalo kuhakikisha kila mgonjwa anapata huduma bora. Tutakujulisha mara tu tutakapopata taarifa za binti yako."
Hersi hakukubaliana na majibu hayo, lakini aliamua kurudi pembeni huku akiendelea kusubiri kwa shauku kubwa. Aliwaambia walinzi wake, "Hakikisheni mnatafuta njia yoyote ya kunipa taarifa za Moreen. Sitaki kukaa hapa bila kujua kinachoendelea."
Wakati huo, ndani ya wodi, madaktari walikuwa tayari wameanza matibabu kwa wakati mmoja kwa Moreen na Zavian. Ndani ya wodi hiyo, hatima ya maisha yao ilianza kufungamanishwa kwa njia ya ajabu.
SIMULIZI: SINCE WE MEET
MTUNZI: SUMAIYA MWENDO
SPONSORED BY: TUPO HAPA. COM
SEHEMU YA: 08
Hospitali ya Ramón y Cajal iliendelea kupokea majeruhi kutoka kwenye ajali ya ndege, huku korido zake zikiwa zimejaa watu waliokuwa wakihangaika kupata taarifa za wapendwa wao. Ndani ya wodi ya wagonjwa mahututi, Moreen, ambaye hali yake ilikuwa imeimarika kidogo, alihamishwa kimyakimya kwenda hospitali nyingine kwa maagizo ya idara ya usimamizi wa hospitali. Uhamisho huo ulifanywa haraka ili kupunguza msongamano wa wagonjwa. Walihamishwa wagonjwa wengi akiwemo yeye.
Hersi, aliyekuwa akihangaika kwa muda mrefu kusubiri taarifa za binti yake, hakupewa taarifa kuhusu uhamisho huo. Aliendelea kusimama kwa hasira kwenye eneo la mapokezi huku akihisi kuwa muda unamponyoka. Mwishowe, alimsogelea mmoja wa wauguzi waliokuwa wakihudumia wodi ya wagonjwa mahututi.
"Nataka kumuona binti yangu sasa hivi! Nilikuja hapa kwa haraka nikiwa na matumaini ya kumpata, lakini kila ninapoeleza sijapata msaada wowote. Yuko wapi Moreen?" aliuliza kwa sauti ya ukali.
Muuguzi huyo alijaribu kumtuliza kwa heshima. "Samahani sana, mheshimiwa. Tumekuwa tukifanya kila jitihada kushughulikia idadi kubwa ya majeruhi hapa. Wagonjwa wengine wamehamishwa kwenda hospitali nyingine kupunguza msongamano."
Hersi alihisi moyo wake ukipasuka. "Unamaanisha nini? Binti yangu amehamishwa pia? Kwa nini hamkuniambia?"
"Samahani, mheshimiwa. Tulipokea maagizo kutoka kwa uongozi wa hospitali. Wagonjwa waliokuwa na nafuu kidogo walipewa nafasi ya kuhamishiwa hospitali zingine ili kuhakikisha matibabu yanaendelea kwa ufanisi," alijibu muuguzi kwa unyonge.
Hersi alipiga hatua mbili mbele kwa hasira. "Sasa niambie, amepelekwa hospitali gani?"
Muuguzi alitoa orodha ya hospitali zilizokuwa zimepokea wagonjwa wa uhamisho. "Tumewahamisha baadhi ya wagonjwa kwenda Hospitali ya Gregorio Marañón, nyingine ni Hospitali ya La Paz, na pia Hospitali ya Severo Ochoa."
Hersi alichukua orodha hiyo haraka na kuwaamuru walinzi wake. "Tuondoke. Hakuna hata sekunde moja ya kupoteza. Moreen lazima apatikane!"
Safari ya Hersi ilianza mara moja. Alitembelea hospitali moja baada ya nyingine, akiingia kwenye mapokezi na kuwauliza wauguzi maswali yaleyale. "Je, kuna mgonjwa aliyeletwa hapa hivi karibuni? Jina lake ni Moreen Hersi."
Hospitali ya kwanza aliyoenda haikuwa na taarifa. "Samahani, mheshimiwa. Hakuna mgonjwa mwenye jina hilo katika orodha yetu," muuguzi mmoja alimwambia.
Hospitali ya pili pia haikuleta majibu yoyote mazuri. Kadri alivyohangaika, hasira na hofu ziliendelea kumtawala. "Hii haiwezekani," aliwaza huku akikanyaga kwa nguvu chini. "Binti yangu yuko wapi?"
Baada ya kutembelea hospitali ya tatu bila mafanikio, Hersi alisimama nje ya lango kuu, akiegemea gari lake huku macho yake yakionyesha kuchoka na kukata tamaa. Mlinzi wake alimkaribia. "Mheshimiwa, tutaendelea kutafuta. Tunaweza kwenda hospitali nyingine kwenye orodha."
Hersi aliinama huku akifunika uso wake kwa mikono. "Ni kama dunia nzima inakataa kunirudishia furaha yangu. Moreen ni kila kitu kwangu... sijui nitakutana na nini zaidi."
Wakati Hersi akiendelea na juhudi zake za kumtafuta binti yake, Zavian alikuwa bado amelazwa katika hospitali ya Ramón y Cajal. Hali yake ilikuwa ikiboreka kidogo kila siku, ingawa bado alikuwa hajarejesha fahamu zake. Madaktari walikuwa na matumaini kwamba ataamka muda si mrefu, kutokana na mwili wake kuonyesha ishara za kuimarika.
Daktari mmoja, akiwa na ripoti mikononi mwake, alimwambia mmoja wa wauguzi wenzake, "Kijana huyu ana nguvu ya ajabu. Ingawa bado hajarejewa na fahamu, mwili wake unaonyesha alama za kupona haraka. Ni jambo la kushangaza, hasa kwa ajali ya kiwango hiki."
Moreen, kwa upande mwingine, alikuwa amefikishwa hospitali ya La Paz, lakini kutokana na hali yake kuwa dhaifu, hakuwa ameweza kutambulika na mtu yeyote. Alikuwa akihitaji uangalizi wa karibu zaidi, huku akiwa amepoteza fahamu kabisa.
Dunia ilikuwa imemuweka Hersi mbali na binti yake, kama adhabu ya kusaliti upendo wake wa awali kwa Helen. Kila sekunde ilivyopita, uchungu wa moyo wake ulizidi. Hersi aliamua kuchukua hatua kali zaidi..
Baada ya siku nyingi za kumtafuta bila mafanikio, Hersi alirudi nyumbani akiwa amejaa hasira. Aliwaita polisi na kuamuru Helen na familia yake wakamatwe mara moja. Alisimama mbele yao kwa macho yaliyowaka hasira na kusema, "Niliwapa nafasi ya kuwa sehemu ya maisha yangu, lakini badala yake, mmekuwa chanzo cha maumivu yangu. Helen, unajua nini? Sasa hivi utalipa kwa kila kitu ulichoharibu. Utaishi na majuto mengi sana."
Helen alilia huku akijaribu kujitetea. "Hersi, tafadhali nisikilize! Sikujua haya yangetokea. Sikukusudia—"
Hersi alimkatisha kwa mkono, akimwonyesha kidole cha onyo. "Nenda ukateseke kama ulivyonitesa mimi. Mungu akiamua, binti yangu atarudi. Lakini wewe, Helen, umenipoteza milele."
Majonzi ya Hersi hayakuwa na mwisho. Dunia ilionekana kama giza lisilo na matumaini, huku moyo wake ukipasuka kwa upweke na huzuni. Wakati huo huo, hatima ya Moreen na Zavian iliendelea kushikiliwa na mikono ya madaktari, wakati ulimwengu wao ukitafuta mwanga wa matumaini ya kuishi tena.
ITAENDELEA..........
SOMA MAELEKEZO
Bonyeza hi "Soma Kitabu" kisha itakupeleka kwenye fomu yaku login, hakikisha ume login na namba uliyojiunga nayo ndipo utaendelea sasa kusoma kitabu chote