SIMULIZI: SINCE WE MEET
MTUNZI: SUMAIYA MWENDO
SPONSORED BY: TUPO HAPA. COM
SEHEMU YA: 16
Usiku ulitulia, lakini ndani ya hoteli ya kifahari, mawimbi ya hasira yalitawala kwenye chumba cha mkutano. Bwana Harry, Madam Morena, na Tesla walikuwa wameketi kwenye meza moja, kila mmoja akiwa na sura ya hasira na kukata tamaa. Kila mara, macho yao yalikutana kwa ukali huku wakijaribu kuamua hatua ya kuchukua dhidi ya Zavian na msichana aliyeharibu mipango yao.
Tesla, alitetemeka kwa hasira, aligonga meza kwa nguvu na kusema, “Sihitaji hata kumfahamu huyo msichana sana! Lakini ikitokea nikakutana naye, hasa tukiwa wawili tutofauti na leo, nitahakikisha anajuta! Nitamfundisha adabu!”
Bwana Harry, akionekana kama mtu aliyeshindwa kuelewa kilichotokea, alikunja uso kwa huzuni na kusema, “Huyo msichana mdogo! Eti anathubutu kunizaba kofi mbele ya Zavian na msaidizi wake? Hana adabu hata kidogo! Siwezi kuvumilia! Lazima kuna kitu anamfanyia Zavian. Huenda…” alinyamaza kwa sekunde akijaribu kuweka mawazo yake sawa.
Kauli hiyo ilimpa Madam Morena wazo. Akainuka kidogo kutoka kwenye kiti chake, akiwatazama wenzake kwa macho makali yenye kujaa uhakika. “Kwa nini tusifanye jambo?” aliuliza kwa sauti ya chini lakini yenye msisitizo.
Bwana Harry alikodoa macho. “Jambo gani unadhani tunapaswa kufanya?” aliuliza kwa shauku huku akijaribu kuelewa.
Tesla alitikisa kichwa kwa hasira, akasema kwa dhati, “Sihiitaji pesa kwa sasa, Madam Morena. Ninataka kumkomesha huyo Moreen Hersi! Nimchape kwa hasira, nimpe adhabu ya kudumu! Ambayo itamkumbusha uwepo wangu hadi mwisho wa maisha yake"
Madam Morena alitabasamu kwa kijicho, tabasamu lenye hila ambalo lilionesha alikuwa tayari amepata mpango wa uhakika. “Basi, tusikilizane kwa makini. Huu ni mpango wangu: Tumvute Zavian kwenye mtego wetu. Mnaonaje kama tukimpata mtu ambae, ni wa katibu zaidi na Zavian alafu Tumpatie dawa za kumvuruga akili kidogo kidogo Zavian bila yeye kujua, na wakati huo huo tuhakikishe dawa hizo zinapatikana kwa Moreen. Watu waone kama ni Moreen anayemfanyia vitu vya ajabu Zavian, na hata Zavian mwenyewe awe na shaka naye.”
Tesla na Bwana Harry walimtazama Morena kwa mshangao, wakiwa kimya kwa muda, wakijaribu kuelewa undani wa mpango huo.
“Kwa nini iwe hivyo?” Tesla aliuliza hatimaye, ingawa sauti yake ilionesha alikuwa tayari kushawishika.
Madam Morena aliendelea, “Kwa sababu itasaidia kuwavuruga wote wawili. Na siyo tu hilo – wakati watu wakiendelea kushuku kuwa Moreen ni mwenye tamaa ya mali na hatari kwa Zavian, sisi tunatumia fursa hiyo kuchota pesa kutoka KMC International polepole. Sio lazima tuimiliki kampuni, tunaweza kuanzisha kampuni nyingine kwa mgongo wa KMC International.”
Kimya kilitawala kwa sekunde chache. Halafu Tesla alitabasamu taratibu, tabasamu ambalo lilikuwa na mchanganyiko wa chuki na msisimko. “ Madam Morena, wazo lako ni zuri kweli tufanye hivyo na sio lazima tumililk KMC bali tunaweza kuwa na kampuni yetu kupitia KMC. Huyo binti Moreen atajua kuwa mimi Tesla si mtu wa kuchezea.”
Bwana Harry alitikisa kichwa kwa furaha, akasema, “Ni mpango mzuri sana, Morena. Hakika hujawahi kuwa msuka mipango bure. Na nakuahidi, nitahakikisha mpango huu unaenda vizuri. Zavian hatajua kilichomkuta mpaka awe ameharibikiwa kwa kila kitu.”
Watatu hao walikubaliana kwa pamoja kwamba wangeutekeleza mpango wao mara moja. Walipongezana, kila mmoja akijihakikishia kuwa ushindi ulikuwa mikononi mwao. Tesla alikuwa na kisasi kikubwa sana haswaaa kwa upande wake kwa sababu, Moreen alimsukuma sakafuni na kumdhalilisha, tena mbele ya Z mwanaume ambae alim crush kwa muda mrefu sana.
☆☆☆☆☆☆
Upande wa pili Zavian alimsindikiza Moreen chumbani ili akaoge, Baada ya kumwonyesha bafu, Zavian alikaa sebuleni akimsubiri. Moreen alionekana mwenye furaha alipoingia bafuni, lakini baada ya muda, sauti ya maji ilipotulia, Zavian aliamini kila kitu kilikuwa sawa na Moreen yupo bize anaoga zake. Alijikuta akimfikiria Moreen alivyobadilisha maisha yake kwa muda mfupi, hivi kweli yeye ni wa kuoa msichana wa aina ya Moreen? Hii ilikuwa ni haiaminiki, sauti ya mlango ilivuruga fikra zake.
Ni Martin. Aliingia ndani ya nyumba akiwa na tabasamu la kiaina, Martin alimpita Zavian na kumtazama kwa dharau kisha akaketi. “Dah! Z, sasa kweli umefikia hatua hii?wewe hapo Bishoo la maana kukaa kwenye kiti cha magurudumu? Wewe si ulikuwa mtu wa kupiga watu mitama wewe?” Martin alisema huku akicheka, macho yake yakimkagua Zavian vizuri zaidi.
Zavian alikasirika. “Huna akili, Martin! Mimi ni kiwete kwa sasa, hali yangu inatia huruma sana. Badala ya kuniombea nifanikiwe, unanishusha morali! Niache bhana, na hata sijui ni kwa nini umekuja hapa”
Martin alitikisa kichwa, kicheko kilimtoka kwa nguvu zaidi. “Wewe ni tofauti, Z. Viwete wengine wanatia huruma. Lakini wewe? Unachekesha! Nadhani miguu yako imeamua kuchukua mapumziko zaidi hapa Hispania baada ya kukimbia sana miaka yote ya umri wako Zavian Karama. ”
Zavian hakutaka kuendelea. Aliweka mikono kichwani na kusema kwa kujionea huruma sana. “Mungu, kwa nini ulinipa marafiki wa aina hii? Martin na Enzo – hawa sio watu kwangu maana hawa ni majanga juu ya majanga! Mungu baba asante kwa baraka za marafiki wape na wengine!."
Wakati huo huo, mlango wa sebuleni ulifunguliwa kwa kishindo, na Enzo akaingia kama upepo. Alirusha mpira aliouleta, ambao ulivuruga kabisa utulivu wa chumba hicho. Mpira ulitua kwenye sahani ya matunda aliyokuwa ameibeba Lolita, mfanyakazi wa ndani wa Zavian, na sahani hiyo ikavunjika vipande vipande sakafuni.
Lolita alishtuka na kuachia kilio kidogo cha hofu. Martin na Zavian waligeuka kumtazama Enzo kwa mshangao. Enzo, kijana mtanashati wa Kihispania lakini mwenye tabia zisizoeleweka, alikimbia kwa haraka kumsaidia Lolita kuokota vipande vya sahani hiyo. “Samahani sana, Lolita! Sikukusudia. Tafadhali unisamehe.”
Lolita alijaribu kutabasamu, akasema, “Usijali, ni sawa.”
Enzo alimsogelea zaidi, sauti yake ikiwa ya heshima. “Unapaswa kuacha kujiona kama mfanyakazi wa ndani tu. Wewe ni mwanamke wa thamani! Usione haya unapopewa heshima.”
Lolita alitabasamu kweli. Katika miaka yake ya kufanya kazi hapo, hakuna mtu aliyewahi kusema hivyo kwake. Enzo alimpa vipande vya sahani na kumwambia awe makini zaidi, kisha akarudi na kuketi kwenye sofa.
Lakini kabla ya kuanza mazungumzo, walihisi sauti ya kilio cha mwanamke ikitokea chumbani. “Z! Macho yangu! Macho yangu yanawasha!”
Martin aligeuka kumtazama Zavian huku akicheka kwa sauti. “Z, huyo ni mwanamke wako tena? Mzee wa totoz bado hujabadilika!”
Zavian alikasirika kidogo na kujibu kwa msisitizo, “Huyu si kama hao wa zamani. Huyu ni mke wangu!”
Enzo, aliyekuwa akinywa maji, alijikuta akiyatema nje kwa mshangao. “Z, umesema nini? Umeoa? Haiwezekani! Au kuna kitu sikijui hapa?”
Martin alicheka sana huku akitikisa kichwa. “Hata hivyo, kila mtu anaweza kuoa, lakini sisi? Hilo hata halijawahi kuingia kwenye mawazo yetu. Hahaha!”
Zavian hakutaka mjadala zaidi. Alinyanyuka ghafla kutoka kwenye kiti cha magurudumu, hatua iliyomshangaza Lolita lakini sio rafiki zake walijua alikuwa akiigiza hali ya ulemavu kwa sababu zake binafsi. Bila kusema neno, alielekea chumbani alipokuwa Moreen.
Alipofika chumbani, mlango wa bafu ulikuwa wazi. Moreen alikuwa ndani, akijipikicha macho yake huku akilia kwa sauti. Kibaya zaidi, hakuwa amevaa kitu chochote mwilini. Zavian alishtuka sana baada ya kumuona, moyo wake ulipiga kwa kasi isiyoeleweka. Alifunga mlango haraka, huku akiwa na joto la aibu na hofu.
“Moreen, unalia nini? Mbona hujavaa hata nguo?” aliuliza kwa sauti iliyokuwa na mchanganyiko wa hasira akijaribu kujizuia.
Moreen alilia kwa nguvu zaidi, “Macho yangu yanawasha sana! Naona kama yanatoka nje! Nisaidie, Z!”
Zavian alikumbwa na wimbi la mawazo. Alijishika kifua huku akiwaza, Kwa mfano, nikishindwa kujizuia hapa? Huyu ni kama mtoto mdogo kiakili, itakuwaje sasa? Maana huu utakuwa sawa na ubakaji? Mungu wangu, niokoe na majaribu!
Alisogea karibu na mlango wa bafu, lakini hakutaka kuangalia zaidi. “Subiri. Nitakuletea maji ya baridi. Usifanye lolote, usifikiche macho yako sawa?” alisema kwa sauti iliyojawa na wasiwasi na tahadhari.
Moreen alikubali kwa kichwa tu, lakini bado alionekana kuwa na maumivu.
ITAENDELEA..............
SIMULIZI: SINCE WE MEET
MTUNZI: SUMAIYA MWENDO
SPONSORED BY: TUPO HAPA. COM
SEHEMU YA: 17
Zavian alikaa nje ya mlango wa bafu kwa muda, akiwa na mawazo mengi. Alijikuta akipumua kwa nguvu, akikumbuka hali aliyomkuta nayo Moreen. "Sina namna, ni lazima nimsaidie," alijisemea kwa sauti ya chini, kisha akaingia bafuni kwa tahadhari.
Akiwa amefumba macho, alisogea karibu na Moreen, akamgusa kichwani kwa uangalifu. "Moreen... ni mimi, Zavian. Nitakusaidia," alisema kwa sauti ya upole. Moreen, akiwa bado na hofu, aliung'ang'ania mkono wake, machozi yakitiririka. "Usiniache, Z... macho yangu... yananiuma sana," alilia kwa uchungu.
Zavian alikaza moyo. "Nitakusaidia. Ni lazima uamini hilo mimi niko hapa kwa ajili yako," alisema huku akifumbua macho na kuanza kumuosha kwa uangalifu. Alihakikisha hakuna povu lililobaki mwilini mwake, alitumia maji ya vuguvugu na kwa upole wa hali ya juu alimsafisha macho yake huku akimpuliza. Hata hivyo, kila alipomgusa, mwili wake ulijibu kwa hisia tofauti. Alijikuta akihema kwa haraka, akijaribu kujizuia na tamaa iliyokuwa ikizidi kumzonga.
Mara ghafla, Moreen alimkumbatia Zavian shingoni, uso wake ukiwa karibu mno na wake. "Asante kwa kunisaidia," alisema kwa sauti ya chini, macho yake yakimwangalia Zavian moja kwa moja.
Zavian alihisi kana kwamba dunia imesimama. Mapigo ya moyo wake yaliongezeka kwa kasi. "Moreen..." alijaribu kusema, lakini kabla hajamaliza, mwili wake uliisaliti akili yake. Alimshika kiunoni na kumsogeza karibu zaidi, kisha akambusu midomo yake kwa upole lakini kwa shauku.
Moreen alishtuka kwa sekunde chache, lakini mshangao wake uligeuka furaha. Busu lile lilikuwa la kipekee, na licha ya hali yake, aliweza kulihisi. Mkono wake mmoja ulienda nyuma ya shingo ya Zavian, alijikuta akimrudishia busu hilo.
Lakini ghafla, Zavian alishtuka kana kwamba ameguswa na umeme. Alijitoa haraka kutoka kwenye busu hilo, akageuka na kuchukua taulo, kisha akampatia Moreen huku akijaribu kutoangalia upande wake. "Hii... hii haipaswi kutokea," alisema kwa sauti ya kujikaza, akionekana mwenye hatia.
Moreen alitabasamu kimyakimya, akijifunika kwa taulo na kutulia. Zavian, kwa upande wake, alitoka bafuni kwa haraka, akijaribu kupoteza mawazo yaliyokuwa yakimtesa. Alienda kukaa kwenye sofa, akaweka mikono kichwani, akijiuliza kimoyomoyo, "Ninafanya nini? Hii so sahihi."
Baada ya muda, Moreen alitoka bafuni, nywele zake zikining'inia na matone ya maji yakimdondoka. Alitembea polepole, kisha akamwambia, "Zavian, nataka nguo za kuvaa."
Zavian alikumbuka kwamba hakuwa amemnunulia nguo zozote bado. Aliinuka taratibu, akachukua baadhi ya tisheti zake na suruali zilizokuwa na kamba akampatia ili zitoshee kiuno chembamba cha Moreen. "Hizi zitakufaa kwa sasa," alisema huku akimpatia.
Baada ya Moreen kuvaa, Zavian alisogea karibu naye na kumpeleka mbele ya kioo. Alikausha nywele zake kwa kitambaa laini, kisha akatumia mashine ya kunyoosha nywele. Moreen alitulia, akimwangalia Zavian kwa shukrani.
"Umependeza sana," Zavian alisema bila kujizuia, kisha akaongea kwa haraka, "Bado unahitaji nguo nzuri. Tutaenda dukani sasa hivi."
Moreen alitabasamu kwa furaha, akionekana mwenye kuridhika. Zavian alimtazama tena, akifikiria jinsi uzuri wake ulivyokuwa wa kipekee hata katika hali yake. "Nitamlinda... na nitahakikisha anakuwa salama mara zote, ni mwanamke mzuri na anastahili kila zuri."
☆☆☆☆
Baada ya Moreen kujiandaa, Zavian alimsindikiza hadi mlangoni kwa macho, akitazama jinsi alivyopendeza hata kwa mavazi ya kawaida aliyomvalisha. Wakiwa njiani kuelekea sebuleni, Zavian alimsihi kwa sauti ya upole, "Kabla hatujafika, nataka uelewe kuwa wale ni rafiki zangu, Martin na Enzo. Hakikisha unawatendea kwa adabu, hata kama watakuwa na maoni tofauti au kunisema vibaya, usiwakasirikie wala kuwazaba vibao, sawa?"
Moreen alimtazama kwa uso wa kutokuamini na kuuliza kwa sauti ya utulivu, "Adabu ni nini?"
Zavian alitulia, akijaribu kufafanua kwa lugha rahisi, "Adabu ni kuwa mpole, kuheshimu watu, na kutojibizana vibaya hata kama unahisi wamekukosea." Moreen alitikisa kichwa kwa kuelewa, ingawa macho yake yalionyesha maswali machache ambayo hakuyatamka.
Walipofika sebuleni, Martin na Enzo walinyamaza ghafla. Macho yao yaliganda kwa mshangao, wakimtazama Moreen. Urembo wake ulionekana wa kipekee, kana kwamba alikuwa ametokea kwenye hadithi za kifalme. Zavian alimsogelea karibu, akimshika kiunoni kwa utulivu na kusema kwa sauti ya furaha, "Huyu ni mke wangu, Moreen."
Martin na Enzo walitabasamu na kuitikia kwa ukarimu, wakimpongeza Zavian, "Hakika umepata mwanamke mzuri sana, Z. Hongera sana, kaka." Moreen alikumbuka maelezo ya Zavian kuhusu adabu na akawajibu kwa upole, "Asante sana kwa kunipokea vizuri."
Mazungumzo yaliendelea kwa furaha, huku Martin na Enzo wakimsifia Moreen kwa jinsi alivyo mrembo na mwenye tabia nzuri. Zavian alitabasamu kwa kuridhika, lakini alihisi Moreen alikuwa akijaribu sana kuwa mkamilifu mbele ya wageni, jambo lililomfanya ajivunie zaidi. Hakuonyesha dalili zozote za uchizi wake.
Baada ya muda, walihamia mezani kwa ajili ya kupata chakula. Wakati kila mtu alipoanza kula, Moreen alikunja uso, akanuna kwa dhahiri. Zavian alimtazama kwa macho ya maswali. "Kuna nini, mpenzi wangu?" aliuliza kwa sauti ya upole.
"Nataka burger," Moreen alijibu kwa sauti ndogo lakini ya ukaidi, alishika uma wake bila kuigusa sahani yake.
Zavian alitabasamu kwa ustahimilivu, akainuka kidogo na kumgusa kichwani kwa upole. "Moreen, wewe ni mwanamke mzuri sana, lakini ukililia burger kila wakati, utakuwa msichana mbaya. Na mimi sitaki uwe msichana mbaya," alisema kwa sauti ya utani lakini yenye upendo mwingi.
Martin na Enzo waligeuka kumtazama Zavian kwa mshangao. "Huyu Sharukh Khan ametoka wapi ghafla?" Martin aliuliza kwa kejeli, lakini Zavian aliwapuuza na kuendelea kumwangalia Moreen kwa tabasamu.
"Fanya hivi, mpenzi. Kula chakula chako vizuri, unywe na juisi yako hii tamu, alafu tutakapotoka kununua nguo, nitakununulia burger. Tutakula pamoja, sawa?" alisema Zavian kwa upole wa hali ya juu.
Moreen aliposikia hivyo, uso wake ulibadilika mara moja. Alitabasamu kwa furaha, akasimama haraka na kumkumbatia Zavian kwa nguvu. Kisha, bila aibu, akambusu usoni na kusema kwa sauti ya furaha, "Asante sana, Darling. Nakupenda!"
Martin na Enzo walibadilishana macho, ishara kwamba waliona kuna kitu hakiko sawa na Moreen. "Z, huyu mke wako yupo sawa kweli?" Enzo aliuliza kwa tahadhari, lakini Zavian alitabasamu tu.
"Yuko sawa kabisa," alisema kwa sauti ya kujihami, kisha akaongeza, "Sasa hebu tuendelee kula, chakula kikiwa bado cha moto."
Walirudi kwenye chakula, lakini Zavian alibaki akimwangalia Moreen kwa upendo mwingi. Alijua hali yake haikuwa ya kawaida, lakini moyo wake ulimhakikishia kwamba alikuwa amefanya uamuzi sahihi kumchagua kama mke wake.
SIMULIZI: SINCE WE MEET
MTUNZI: SUMAIYA MWENDO
SPONSORED BY: TUPO HAPA. COM
SEHEMU YA: 18
Baada ya kumaliza chakula, Zavian, Moreen, Enzo, na Martin walisimama tayari kwa safari yao. Enzo na Martin walikuwa na ratiba ya haraka, hivyo walionekana kutokuwa na muda wa kukaa muda mrefu. Enzo, hata hivyo, alimwangalia Moreen kwa macho ya shaka. Hali ya Moreen ilikuwa imechochea hisia za wasiwasi kwake, na aliamua kuzungumza moja kwa moja na Zavian.
"Z, mimi na wewe bado hatujamalizana," Enzo alisema kwa sauti ya upole lakini yenye msisitizo.
Zavian alitabasamu, akimpatia Enzo ishara ya utulivu. "Tutazungumza baadaye, rafiki yangu," alisema huku akimpa Enzo ishara ya simu.
Enzo alitikisa kichwa kwa kukata tamaa. "Sawa, lakini kumbuka, Z. Hili halijaisha."
Enzo na Martin waliondoka huku wakibadilishana mazungumzo ya chini kwa chini, wakihisi kwamba Moreen alikuwa na hali fulani ya kipekee ambayo haikufahamika kirahisi. Wakati huo, Henry alifika na gari. Zavian na Moreen wakahamia kwenye gari la Henry, kisha safari yao ya kuelekea shopping ikaanza.
Walipofika kwenye duka kubwa la nguo, Moreen aliangua tabasamu kubwa alipoyaona mavazi yaliyokuwa kwenye rafu. Ghafla, alikimbilia sehemu ya nguo za watoto na kuanza kuzivuta huku akizishika kwa nguvu, macho yake yakiwa yamejaa furaha isiyoelezeka.
Zavian alifuatilia kwa utulivu, akauchukua mkono wake polepole na kumwambia kwa sauti ya upole, "Moreen, usifanye utundu. Hizi nguo sio za kwako."
Moreen alikunja uso kwa huzuni, akanuna kwa dhahiri. Zavian akasogea karibu na kumshika begani. "Mtoto mzuri, usinune. Ukifanya hivyo, unakuwa msichana mbaya, na mimi sitaki uwe hivyo. Njoo, twende tuangalie nguo nzuri za wasichana wakubwa kama wewe. Ukivaa hizi, utapendeza sana."
Moreen aliitikia kwa kichwa na kumsukuma Zavian aliyekuwa amekaa kwenye wheelchair. Wakaenda hadi sehemu ya nguo za wanawake.
Walipofika kwenye rafu za nguo za kisasa, Moreen alizama ki hisia katika mavazi mazuri yaliyokuwa mbele yake. Mkono wake ulianza kushika vazi moja baada ya lingine, lakini ghafla, alisimama bila kutarajia. Macho yake yalijaa ukungu wa mawazo, na alishikilia kichwa chake kwa mkono mmoja. Mavazi yalimfanya ajikumbuke yeye kama Moreen wa enzi hizo.
Picha za zamani zilianza kuibuka kichwani mwake—siku zile ambazo alikuwa akipendeza, akiwa katika mavazi ya kisasa na maisha yenye thamani. Mawazo hayo yalikuja kwa nguvu, yakamwacha akiwa ameduwaa. Polepole, vidole vyake viliachia nguo alizokuwa ameshika. Kichwa chake kiliegemea upande mmoja, na mwili wake ulianza kuyumba, kana kwamba alikuwa anaelekea kuanguka.
Zavian, aliyekuwa akimsubiri kwa umbali mfupi, alihisi mabadiliko hayo. Bila hata kufikiria kwamba yeye ni kiwete mbele za watu, alisimama haraka kutoka kwenye wheelchair yake, akasahau kabisa kwamba alikuwa akijifanya mlemavu. Alienda moja kwa moja hadi kwa Moreen.
"Moreen!" alimuita kwa sauti ya wasiwasi, akimshika kabla hajadondoka. Aliinua uso wake polepole, akimwangalia kwa macho yaliyojaa huruma.
Moreen aliutazama uso wa Zavian kwa sekunde chache, macho yake yakionyesha mchanganyiko wa maumivu na upendo. Hatimaye, alifumba macho, kichwa chake kiliangukia kifuani kwa Zavian.
Zavian alimsogeza karibu zaidi, moyo wake ukijaa wasiwasi. Henry, aliyekuwa akitazama kwa mbali, alimfuata mhudumu wa duka na kusema kwa sauti ya msisitizo, "Hakikisha nguo zote ambazo Moreen amegusa zinawekwa pembeni. zitalipiwa sasa hivi."
Wakati huo, Zavian alikuwa nje, akiwa amembeba Moreen kwenye mikono yake, alikimbia kuelekea kwenye gari. Uso wake ulikuwa na hofu isiyofichika. Hakuelewa ni nini kilikuwa kimemtokea Moreen, lakini pekee alichojua ni kwamba, alijua kwamba alihitaji msaada wa haraka.
"Henry, fungua mlango wa gari, haraka!" Zavian aliamuru kwa sauti ya dharura.
Henry alifungua mlango mara moja, na Zavian akamweka Moreen kwa upole kwenye kiti cha nyuma. Alikaa pembeni yake, akiweka mkono mmoja juu ya paji lake la uso, akijaribu kumpa utulivu.
"Moreen, nitahakikisha uko salama. Nitakupigania, hata kama sijui ni nini kinakusumbua," aliongea kwa sauti ya upendo.
Safari ya kuelekea hospitali ilianza, Zavian akiwa amemshika Moreen kwa upole huku akimwangalia kwa macho yaliyojaa hisia za mchanganyiko wa hofu na upendo wa kweli.
SIMULIZI: SINCE WE MEET
MTUNZI: SUMAIYA MWENDO
SPONSORED BY: TUPO HAPA. COM
SEHEMU YA: 19
Walipofika hospitalini, Zavian alimnyanyua Moreen haraka na kumpeleka ndani, uso wake ulionyesha hofu kubwa. Wauguzi walimkimbilia mara moja, wakimpokea Moreen kwa tahadhari na kumpeleka moja kwa moja kwenye wodi ya dharura. Zavian alibaki mlangoni, akihisi kama muda ulikuwa umesimama, huku akimuangalia Moreen akipotelea ndani ya wodi.
Henry alijaribu kumtuliza Zavian kwa kumgusa begani. "Atakuwa salama, bosi," alisema kwa sauti ya upole.
Walikaa kwenye kiti cha kungojea huku Zavian akiwa kimya, macho yake yakiwa yamejawa na wasiwasi. Baada ya muda, daktari alitoka, akimkaribia Zavian huku akitabasamu.
"Zavian, nadhani itabidi uanze kufikiria kununua kiti cha kudumu hapa hospitalini," daktari alisema kwa utani wa kirafiki.
Zavian hakutabasamu mara moja. "Kwa nini unasema hivyo, Daktari?" aliuliza kwa sauti yenye mkazo.
Daktari aliketi karibu naye na kusema kwa utulivu, "Kwa sababu Moreen ameanza kurejesha kumbukumbu zake. Ni jambo zuri, lakini ni mchakato mrefu na mgumu. Kila anapopata kumbukumbu mpya, huenda akapitia maumivu ya kichwa au hali kama aliyopata leo. Ni jukumu lako kuhakikisha anapata chakula bora, usingizi wa kutosha, na mazingira tulivu. Kwa sasa, unapaswa kumlea kama mtoto mdogo anayejifunza tena maisha. Kwa sababu kichwa chake ni sawa karatasi tupu. Utachoandika ndani yake ndo kitadumu"
Zavian alikubali kwa kichwa, lakini daktari aliendelea. "Kumbukumbu zake zitakua kwa kasi sana, na ikiwa hatakuwa akihudhuria kliniki mara kwa mara, inaweza kumsababishia matatizo makubwa zaidi."
Kwa sauti thabiti, Zavian alisema, "Nitahakikisha analindwa na anapata matibabu anayohitaji. Sitamwacha mwenyewe hata kidogo."
" vizuri sana Zavian Karama " daktari alimpiga piga begani kisha akainuka kuendelea na majukumu yake mengine.
Baada ya muda mrefu wa kusubiri, Moreen alizinduka polepole. Macho yake yalipotazama usoni kwa Zavian, tabasamu lenye upendo lilitanda usoni mwake.
"Honey," Moreen alisema kwa sauti dhaifu lakini yenye furaha. "Nilizipenda nguo zote ulizochagua kwa ajili yangu."
Zavian alitabasamu kwa furaha na kumsogelea. Aliweka mkono wake polepole kwenye uso wa Moreen na kumkumbatia kwa upendo wa dhati.
Wakati huo, Moreen alimwangalia kwa makini, akionekana kukumbuka kitu muhimu. "Z, ulikuja hapa bila kiti chako cha siri. Ulisema ni siri kati yetu," alisema kwa sauti ya mshangao.
Zavian alihisi moyo wake ukipiga kwa nguvu. Hakujua la kusema. Alikuwa amesahau kabisa kuhusu kujifanya mlemavu alipomkimbilia Moreen pale dukani. Kabla hajapata nafasi ya kujibu, Henry aliingia wodini kwa haraka, akiwa ameshika simu mkononi mwake Uso wake ulionyesha dharura.
"Bosi, angalia hii," Henry alisema huku akimpa simu.
Zavian alichukua simu na kuangalia video ambayo ilikuwa imesambaa mtandaoni. Video hiyo ilionyesha jinsi alivyomkimbilia Moreen na kuacha kiti kwenye duka la nguo, akimuokoa kabla hajadondoka. Kichwa cha habari kilisomeka:
**"Mapenzi Yana Run Dunia: Jamaa Kiwete Apona Kwa Muujiza wa Mapenzi!"**
Zavian aliona maelfu ya maoni na watu wakijadili tukio hilo. Baadhi ya maoni yalikuwa
**"Huu ni muujiza wa kweli! Upendo una nguvu kubwa! Una nguvu kushinda kifo"**
**"Inaonyesha jinsi mtu anavyoweza kujitoa kwa mpendwa wake anae ikaribia hatari, hata. Kama akiwa kwenye hali gani?. Hongera kwao."**
**"Kama kweli alikuwa kiwete, basi hii ni ajabu. Mapenzi ni tiba ya kila kitu!"**
**"Jamani, lakini mbona huyu jamaa anaonekana mzima? Kuna kitu kinafichwa hapa sio rahisi kupona ukiwete mjue."**
**"Zavian ni mfano wa mwanaume anayejali. Tunahitaji wanaume zaidi kama yeye! Sema bahati mbaya hawapatikani ki rahisi**
**"Hii si kawaida, mtu anajifanya kiwete au mapenzi yamemponya? Habari bado inakosa mshiko. Aliepost inabidi atupe mrejeshonini kilitokea baada ya hapo"**
Zavian aliweka simu pembeni, uso wake ukiwa umejaa mshangao na hofu. Mawazo mengi yalimjia kichwani. Je, kuna watu kutoka kwenye kampuni yake ambao wameshaona video hiyo? Hii itakuwaje sasa? Na alipanga iwe siri yake ya muda mrefu?
Alishika kichwa kwa mikono miwili, alijikuta akipumua kwa nguvu. "Hili ni kubwa zaidi kuliko nilivyofikiria," alisema kwa sauti ya chini, akionekana kuzungumza zaidi na nafsi yake.
SOMA MAELEKEZO
Bonyeza hi "Soma Kitabu" kisha itakupeleka kwenye fomu yaku login, hakikisha ume login na namba uliyojiunga nayo ndipo utaendelea sasa kusoma kitabu chote