utangulizi
SIMULIZI: MARRY MY DAD
MTUNZI: SUMAIYA MWENDO
SEHEMU YA: 01
Barabara za Nairobi zilikuwa zimejaa harakati za jioni, magari yakipishana kwa kasi huku jua likitua polepole. Ndani ya eneo la shule ya kimataifa ya **Greenfields**, kelele za watoto waliokuwa wakisubiri kuchukuliwa zilianza kupungua. Sidrath Fafa, binti mdogo wa miaka sita, alikuwa amesimama peke yake akitazama mbali, machozi yalianza kumtiririka. Dereva wake hakuwa amefika, na giza lilikuwa likianza kuingia.
"Baba alisema atanipenda daima… lakini kwa nini ananipa watu wasiojali?" Sidrath alijisemea, akihisi hofu ikimkumba. Ghafla, aliona kivuli cha wanaume wawili wakimkaribia kwa kasi. Akahisi mwili wake ukitetemeka. Hakutaka kusimama. Aligeuka na kukimbia kwa nguvu zake zote, bila kujua alikokuwa anaelekea.
Alikimbia mpaka mtaa wa pili na kuingia kwenye mgahawa uliojaa watu. Kelele za viti na vyombo zilikuwa nyingi, lakini hakuna kilichoweza kumtoa kwenye hofu aliyohisi. Alipokuwa karibu kuanguka kwa uchovu, alimwona msichana mmoja akihudumia wageni, sura yake ikitoa utulivu wa ajabu. Bila kufikiria, Sidrath alimkumbatia msichana huyo kwa nguvu, akasema kwa sauti ya hofu:
"Tafadhali nisaidie! Wanataka kuniteka!"
Zainab Yusuph, mhudumu wa miaka 23, alishtuka lakini akabaki imara. Alimtazama binti huyo mdogo na kisha akageuza macho yake kwa haraka kuwaangalia wanaume waliokuwa wakija kwa kasi kuingia mgahawani. Zainab hakusita. Akiwa na ujasiri usio wa kawaida, alimvuta Sidrath nyuma yake na kusimama mbele ya wanaume hao wawili.
"Mnataka nini kutoka kwa huyu mtoto ?" aliuliza kwa ukali, sauti yake ikikatisha kelele za mgahawa.
"Hakuna kinachokuhusu, tupe mtoto," mmoja wao alijibu kwa hasira.
Lakini Zainab hakuwa tayari kurudi nyuma. Aliwafyatulia glasi iliyokuwa mezani, kisha akashika chupa ya maji kwa mikono miwili. Mapambano makali yaliibuka kati ya Zainab na hao wanaume, na wanaume wale walipoona hamasa ya watu waliokuwa wakimshangilia Zainab, walikimbia bila kugeuka wala kurudi nyuma.
Zainab aliketi chini, akamtuliza Sidrath aliyekuwa anatetemeka. "Usijali, sasa uko salama," alisema kwa sauti laini. Alitoa glasi ya maji na kumpa. "Kunywa kidogo, utakuwa sawa."
Sidrath alikunywa maji huku macho yake madogo yakimtazama Zainab kwa mshangao na shukrani. "Wewe ni shujaa," alisema kwa sauti ya hofu iliyoanza kupungua. "Na… unaweza kuwa mama yangu?"
Swali hilo lilimfanya Zainab kupigwa na butwaa. Kabla hajajibu, Sidrath alimwomba, "Tafadhali, geuka nikupige picha."
Zainab alicheka kidogo, lakini aligeuka kama alivyoombwa. Sidrath alichukua simu yake na kumpiga picha, kisha akatuma moja kwa baba yake, Luqman Fafa, na ujumbe mfupi:
"Baba, tayari nimempata mama. Bado wewe kumpata mke."
Luqman alipokea ujumbe huo akiwa ofisini kwake, kwenye ghorofa ya juu ya jengo la kampuni yake, **Fafa Motors Ltd**. Alifungua picha hiyo na kuona uso wa msichana aliyeonekana mchanga na mwenye tabasamu la uchangamfu. Alitikisa kichwa kwa tabasamu la kejeli.
"Sidrath… ni vituko gani tena hivi?" alisema kwa sauti ya chini, akifunga simu bila kufikiria zaidi.
☆☆☆☆
Baada ya shughuli zake za kutwa, hatimaye Zainab alichukua jukumu la kumrejesha Sidrath nyumbani. Wakiwa ndani ya bajaji ndogo iliyokuwa ikisafiri taratibu kupitia barabara za Nairobi, Zainab alimwangalia binti huyo kwa jicho la huruma. Sidrath, licha ya kutabasamu, alionekana kuwa na uchovu na hisia mchanganyiko usoni mwake.
Walipofika mtaani kwao, Sidrath alimkataza Zainab kufika hadi nyumbani kwao. "Aunt Zena atakuja kunichukua hapa," alisema kwa sauti ya kujiamini. Kisha akatoa simu yake na kumpigia msichana wao wa kazi. Baada ya dakika chache, Zena alifika akiwa na tabasamu la kirafiki.
"Asante sana kwa kumsaidia Sidrath," Zena alisema kwa heshima huku akimshika mkono binti huyo.
"Hakuna tatizo," Zainab alijibu kwa unyenyekevu. Alimtazama Sidrath kwa muda mfupi, kisha akasema, "Kuwa mwangalifu, sawa?"
"Nitakuwa salama. Asante sana," Sidrath alisema huku akimkumbatia Zainab kabla ya kuondoka na Zena. Zainab alitazama nyuma yao kwa muda kabla hajageuka na kuanza safari ya kurudi nyumbani kwake, alikokuwa akiishi na rafiki yake, Thuwaibath.
SIMULIZI: MARRY MY DAD (OLEWA NA BABA YANGU)
MTUNZI: SUMAIYA MWENDO
SEHEMU YA: 02
Endelea.....
Zainab aliondoka moja kwa moja hadi nyumbani kwao, alipofika hakupoteza mda alianza kumsimulia, Thuwaibath kila kiti kilichotokea.
"Naweza kusema leo imekuwa siku ya kushangaza," Zainab alianza kwa sauti yenye mshangao. "Binti mdogo amekuja mbio mbio na kunikumbatia kana kwamba tulikuwa tunafahamiana maisha yetu yote! Nilihisi kama ni jukumu langu kumsaidia wakati huo."
Thuwaibath alishusha pumzi na kusema, "Unajua, kuna vitu vinavyotokea bila sababu ya kueleweka. Lakini hiyo ni ishara kwamba labda kuna jambo kubwa zaidi linakuja mbele yako wewe na huyo mtoto. Wewe ni mtu mzuri, na sidhani kama ni bahati mbaya."
"Lakini, Thuwaibath," Zainab alisema huku akitikisa kichwa, "huyo msichana anaonekana kuwa na utata kidogo. Aliniambia waziwazi kwamba anataka niwe mama yake. Mara ghafla niolewe na baba yake, ungekuwepo ungecheka sana nahisi"
Thuwaibath alicheka. "Labda ni mwanzo wa safari mpya. Huenda binti huyo anataka kukuunganisha na baba yake. Lakini, hebu fikiria—je, upo tayari kuwa mke wa mtu na kuwa mama?"
"Sidhani kama nimewahi kufikiria mama. Kwanza kabisa, sijawahi hata kuolewa! Nitakuwaje mama kabla ya kuwa mke?"
"Si ndo maana akasema olewa na baba yake?" Thuwaibath alisema kisha akaendelea"Kama ni mapenzi ya Mungu, yote yatawezekana. Lakini kwa sasa, tulia na uone tu itakavyokuwa."
" Bhana mi nachukulia kila kitu masihara, mtu unawezaje kumuona tu kwa mara ya kwanza ukamtaka aolewe na baba yako? Yule.bado mtoto kwa hiyo haijui sana dunia" alisema Zainab akaendelea kukunja nguo zake alizokuwa ameanua. Thuwaibath alitikisa kichwa chake akisema labda ni kweli?
☆☆☆
Huku nyumbani kwa familia ya Fafa, Sidrath alikuwa ameketi kwenye sofa kubwa akiwa pamoja na bibi yake, Bi Naima Fafa. Alionyesha picha ya Zainab aliyokuwa ameipiga mapema sana siku hiyo.
"Bibi, huyu ndiye mama ninayemtaka," alisema kwa msisitizo. "Ni mrembo, mchangamfu, na aliniokoa. Tafadhali hakikisha baba anamwoa. Sitaki mama mwingine."
Naima alitabasamu kwa upole huku akiitazama picha hiyo kwa makini. "Ni mrembo kweli kweli," alisema kwa unyenyekevu. "Lakini, Sidrath, hatuwezi kufanya uamuzi haraka haraka. Lazima tumjue zaidi kabla ya kufanya maamuzi makubwa kama hayo."
"Lakini bibi!" Sidrath alisema kwa sauti ya kulalamika. "Mimi tayari nimemchagua. Kwa nini tusifanye kitu sasa?"
Naima alimwangalia kwa upole lakini kwa uthabiti. "Mpenzi wangu, najua unavyohisi. Na nataka ufurahie maisha yako ukiwa na familia kamili. Lakini kuna mambo mengi yanayohitaji kufikiriwa. Hata hivyo, nitakusaidia. Lakini kumbuka, mambo mazuri yanahitaji muda, hayahitaji haraka"
Sidrath alikunja uso kwa huzuni. "Lakini bibi, mimi siwezi kusubiri. Baba kila mara anapuuza mawazo yangu. Na kama hutamisaidia kumshawishi, basi sijui nitafanya nini."
Naima alishusha pumzi ndefu. "Sidrath, nakuhakikishia nitafanya kila linalowezekana. Amini hivyo. Lakini tuanze kwa hatua moja—tumjue kwanza huyu Zainab kwa undani zaidi."
Asubuhi iliyofuata, Bi Naima alimpigia simu Abubakar, rafiki wa karibu sana na Luqman Fafa. Wakiwa wamekaa kwenye mkahawa wa kifahari jijini Nairobi, Bi Naima alimweleza kila kitu kuhusu Zainab na jinsi alivyokutana na Sidrath, kisha akampa picha.
"Abubakar, nataka umfuatilie huyu msichana," alisema kwa sauti yenye mamlaka lakini ya upole. "Nataka tujue zaidi kuhusu maisha yake kabla ya kufanya maamuzi."
Abubakar alitikisa kichwa. "Usijali, mama. Nitahakikisha ninapata taarifa zote muhimu kuhusu huyu Zainab. Ikiwa kweli ni mtu mzuri, nitamshauri Luqman afikirie kuhusu hilo suhala"
Bi Naima alitabasamu kwa shukrani. "Nina imani kubwa na wewe, Abubakar. Huyu msichana anaweza kuwa zawadi kwa familia yetu, hasa hasa kwa Sidrath."
ITAENDELEA............
SIMULIZI: MARRY MY DAD
MTUNZI: SUMAIYA MWENDO
SEHEMU YA : 03
Baada ya siku mbili za uchunguzi, Abubakar alifika kwenye nyumba ya kifahari ya familia ya Fafa kuwasilisha mrejesho wake kwa Bi Naima. Walikuwa wameketi kwenye sebule kubwa yenye mapambo ya kupendeza, huku sauti ya upepo wa unaovuma hadi kwenye dari ikiimba taratibu. Bi Naima alimkaribisha Abubakar kwa heshima, huku akiwa na shauku ya kujua alichogundua.
"Bi Naima," Abubakar alianza kwa sauti ya utulivu, "Zainab ni msichana wa heshima, mwenye bidii, na mrembo sana. Anajua kushirikiana na watu na anaonekana kuwa na roho safi. Kwa kweli, hana sifa zozote mbaya ambazo zinaleta shaka."
Bi Naima alitabasamu. "Unajua, Abubakar, nilihisi tu kwamba Sidrath hakufanya makosa katika uchaguzi wake. Nafurahi kusikia taarifa nzuri kama hizi kuhusu binti huyo. Asante kwa juhudi zako."
Baada ya mazungumzo yao, Bi Naima alijikuta akimpenda Zainab hata kabla ya kukutana naye. Aliamua kumridhia kama chaguo la mjukuu wake na kisha akapanga jinsi ya kumshawishi Luqman.
Upande mwingine wa nyumba hiyo, kwenye chumba cha michezo, Luqman alikuwa akiigiza nafasi ya "jambazi" wa michezo dhidi ya binti yake, Sidrath. Walikuwa wakicheza mchezo wa police kamata mwizi, huku sauti za kelele na vicheko zikijaa chumbani. Sidrath, akiwa na tabasamu pana, aliruka kwa furaha aliposhinda raundi nyingine na kumkamata baba yake.
"Yes baba, nimeshinda tenaa, mimi ni bingwa!" Sidrath alisema kwa sauti ya ushindi.
Luqman alitabasamu. "Sawa, mshindi wangu. Lakini kumbuka, ushindi si kila kitu." Kisha aliongeza kwa utani, "Lakini safari hii nitakushinda, na ushindi wako utaonekana kama jivu."
" hizo ni ndoto za Abunuwasi" alisema Sidrath baba yake akamsogelea
" Abunuwasi ndo nani?"
"Mi namjua sasa baba, nasikiagq tu watu wanasema" Luqman alicheka akamvuta karibu nae.
" au za Alinacha?" Alisema Luqman
" mhh baba! Umemjuaje Alinacha?"
" mi simjui kwani wewe unamjua?"
" mi namjulia wapi sasa nasikia tu watu wakiongea"
" ahahahahaha, baba wewe bado.upo mbali sana na dunia, Alinacha hupo.kwenye wimbo wa zuchu"
" anha kumbe!"
" ndiio"
" huo wimbo unaimbwaje?" Alihoji Luqman
"Ndo kakwambia ataniacha, aa, ee unachekesha sana, hizo ni ndoto za Alinacha, haha, hehe anakudanganya"
" mhh wewe binti unasoma kweli?"
" sasa baba kusoma na kuimba vina husiana kweli?"
" ndio sana"
" mh.hapana, mimi lazima nipate burudani "
Walipokuwa wakibadilisha story, Sidrath alikimbilia kiti na kumwangalia baba yake kwa sura ya uzito.
"Baba, kuna jambo nataka kusema," alisema kwa sauti ya upole lakini yenye msisitizo.
"Sema, binti yangu," Luqman alimjibu huku akirekebisha skrini ya mchezo.
"Nataka umuoe Zainab. Yeye ndiye mama ninayemtaka. Tayari nampenda sana kama mama yangu."
Luqman alikaa kimya kwa muda, kisha akapumua kwa kina. "Sidrath, hilo haliwezekani. Yule msichana... sijui kama ni mzuri kwa familia yetu. Na huenda anapenda pesa zetu, na siyo sisi ujue."
Sidrath alikunja uso, akavimbisha mashavu yake, na kugeuka pembeni kwa hasira. "Baba, wewe huelewi chochote! Yeye ni mzuri, na mimi tayari nimemchagua, kwanza hajui kama tuna pesa wala maisha mazuri."
Luqman alitabasamu kwa utani, akijaribu kumtuliza. "Basi sawa, Malaika wangu, lakini tafadhali usijaribu kunishawishi kuhusu wanawake nisiowaelewa."
Sidrath alisimama ghafla, akasema kwa msisitizo, "Hapana, baba. Nimeamua. Zainab ndiye mama yangu, na nataka awe mke wako. Hilo halibadiliki!" Kisha akaondoka chumbani, akiwa amekunja uso na kurudi kwa bibi yake huku hasira zikiwa bado zimetanda usoni.
Luqman alibaki ameshika kichwa, akijaribu kuelewa kwa nini Sidrath alikuwa amevutiwa sana na huyo msichana. "Huyu Zainab ana nini hasa?" alijiuliza kwa sauti ya chini.
Akiwa bado anafikiria, Abubakar alitokea mlangoni akiwa na bahasha ndogo mkononi. "Luqman," alisema kwa sauti ya utulivu, "hii chukua."
Luqman alizidaka picha zilizotaka kudondoka ndani ya bahasha na kushangazwa na uso aliouona. "Huyu ni nani?" aliuliza huku akimtazama Abubakar.
Abubakar, aliyekuwa akitabasamu, alimjibu, "Huyu ni Zainab. Na ni msichana niliyemchunguza kwa ombi la mama yako."
Luqman alimtazama tena Zainab kwenye picha. Aligeuka kumwangalia Abubakar na kusema, "Kwa nini wamepa msukumo wa kumfanya huyu msichana kuwa mke wangu? Tena wote wawili"
Abubakar alitabasamu kidogo kabla ya kujibu. "Kwa sababu, rafiki yangu, Sidrath tayari kampenda, na ni bahati kupata msichana mwenye tabia kama zake. Ana roho safi, mchangamfu, na anastahili kuwa sehemu ya familia yako kwa sababu mama pamoja na binti yako, wamemridhia. huyu ndiye mtu sahihi wa kuoa."
Luqman alitikisa kichwa huku akijaribu kumwelewa rafiki yake. "Kwa nini sasa usimuoe wewe kama unavyomsifia?"
Abubakar alicheka." Unajua kabisa nina mwanamke, hata hivyo ni kwa sababu nafikiri yeye ana nafasi kubwa zaidi ya kuwa sehemu ya familia hii kwa sababu Sidrath wako anampenda sana. Na bila shaka, wewe ndiye unayestahili kuwa mume wake."
Luqman alikaa kimya kwa muda, akimfikiria Zainab zaidi. "Haya, ngoja nifikirie." Aliwaza tu afanye nini kabla hajaamua chochote, ki ufupi yeye anamuona wa kawaida mno.
ITAENDELEA..........
SIMULIZI: MARRY MY DAD (OLEWA NA BABA YANGU)
MTUNZI: SUMAIYA MWENDO
SEHEMU YA: 04
Endelea.........
Wakati huo, Zainab hakuwa na habari kuhusu kinachoendelea. Ndo kwanza alikuwa zake Ofisini kwake, alikuwa bize akihudumia wateja waliokuwa wakijazana kwa sababu ya uchangamfu wake wa kipekee pale kazini pamoja na huduma zao nzuri. Alikuwa akiimba wimbo mtamu uliowafanya wateja wake kufurahia muda waliokuwa wakiutumia hapo.
"Zainab, una sauti nzuri sana," mmoja wa wateja alisema.
"Asante," Zainab alijibu kwa tabasamu, aliwashukuru watu kwa kila neno jema alilopewa. Ki ufupi alikuwa binti mmoja mzuri sana anaejali watu, hata kama hakuwajua ndo maana watu walimkubalu mno. Alifanya kazi kwa bidii sana na kupeleka hesabu kamili za mchana kwa Meneja wake.
Majira ya jioni, Zainab alikuwa anamalizia ratiba yake ya siku. Harufu ya vyakula vitamu, sauti za wateja wakiongea, na hekaheka za wahudumu walioshughulika vilijaza hewa nzuri hapo. Zainab Alikuwa amechoka lakini aliridhika na kazi yake kwa siku hiyo. Wakati huo, mlango wa mgahawa ulifunguliwa taratibu, na Thuwaibath, rafiki yake wa karibu, aliingia.
Thuwaibath, ambaye hufanya kazi katika "Pharmatech Pharmacy" iliyopo katikati ya jiji, alimtazama Zainab kwa tabasamu pana. “Leo umechoka sana, eeh?” aliuliza huku akimsogelea.
Zainab alitabasamu kwa uchovu. “Umejuaje? Hii siku imekuwa ndefu kweli, lakini Namshukuru Mungu kila mteja anafurahia huduma.”
“Hilo ndiyo muhimu,” Thuwaibath alimjibu, “Lakini sasa tutaongea tukitoka hapa. Hebu maliza shughuli zako tupange bajeti zetu.”
Baada ya kuwapungia mkono wateja wa mwisho, Zainab alimfuata meneja wake, Bwana Hassan, kumuaga na kuchukua ujira wake wa siku hiyo.
“Zainab, umefanya kazi nzuri sana leo,” Bwana Hassan alimpongeza huku akimkabidhi bahasha. “Endelea na juhudi hizi hizi.”
“Asante sana, Bwana Hassan,” Zainab alimjibu kwa unyenyekevu.
Wakati huo huo, Thuwaibath alimsubiri kwa uvumilivu nje ya mlango wa mgahawa. Walipotoka, walishikana mikono na kuanza safari yao ya kuelekea nyumbani. Barabara za Nairobi zilikuwa na shamrashamra nyingi za jioni, watu walirejea nyumbani, wengine walifanya biashara za mwisho mwisho.
“Haya sasa,” Thuwaibath alianza mazungumzo, “Pesa zetu za mwezi huu tunazitumiaje?”
Zainab alitabasamu. “Unajua, kodi yetu imekaribia kuisha, na ndani pia kuna vitu muhimu vimepungua. Nafikiri tununue mchele, mafuta, na sabuni kwanza. Halafu, kama kuna salio, tunaweza kuweka kidogo kwenye akiba.”
Thuwaibath alikubaliana naye. “Ndio, na pia tunahitaji kununua blanketi jipya. Baridi imekuwa kali sana siku hizi.”
“Kweli kabisa,” Zainab alijibu huku wakitembea. “Hii miezi huwa migumu, lakini tunashukuru kwa kila kidogo tunachopata.”
" tatizo lako Zainab nikikwambia olewa ujipunguzie majukumu. Wewe hutaki haya bhana"
" mbona we hujaolewa hebu niache kwanza, kichwa changu kimejaa uchovu"
" umeona unavyosema hapa, ndo huwa unawajibu wanaume hivyo pia" alisema Thuwaibath Zainab akacheka.
" Sway ujue wewe akili zako ni mwaka robo, hebu achana na mimi hao wanaume kwani hawana kwao?"
Mazungumzo yao yaliendelea hadi walipofika nyumbani kwao, walikuwa wamechoka kiasi kwamba kila mtu alikimbilia kujitupa kitandani.
☆☆☆☆
Usiku ulipoingia, Luqman alikuwa amemlaza binti yake Sidrath baada ya kumpa hadithi ya usiku. Alipokuwa akitoka chumbani kwake, alimkuta mama yake, Bi Naima, akiwa amesimama kwenye mlango wa chumba chake, alionekana kuwa na jambo la kuzungumza.
“Mama, mbona hujalala bado?” Luqman aliuliza kwa mshangao.
“Luqman, kuna jambo muhimu nataka tuzungumze kabla sijalala,” Bi Naima alijibu kwa upole.
Luqman alikubali. “Sawa, twende tukae kwenye bustani.”
Walielekea kwenye bustani ya nyumba hiyo, sehemu tulivu iliyozungukwa na maua yanayonukia vizuri. Hewa ilikuwa baridi, na Zena, mfanyakazi wao wa ndani, aliwaletea vikombe viwili vya kahawa ya moto.
Bi Naima alikunywa funda la kahawa kabla ya kuanza mazungumzo. “Luqman, unajua kwamba wakati mwingine ni muhimu kufanya jambo ambalo linaweza kuonekana gumu kwa sasa lakini linaweza kuleta faida kubwa baadaye?”
Luqman alimwangalia mama yake kwa macho ya udadisi. “Mama, unajaribu kusema nini hasa?” maana tayari Luqman ali ihisi mada ya mama yake.
“Nataka uzingatie kuhusu suhala la kumuoa Zainab,” Bi Naima alisema moja kwa moja.
Luqman alishusha pumzi nzito. “Mama, siwezi kufanya hivyo. Kwanza, simjui vizuri. Pili, sijui kama ana nia ya dhati au kama anapenda mali zetu zaidi nawezaje sasa?.”
Bi Naima alimwangalia mwanawe kwa upole lakini kwa uthabiti. “Luqman, nakuelewa, lakini nakusihi unisikilize. Kama mama yako, nakuomba ufanye jambo hili kwa ajili yangu. Nikiwa hai, nataka kuona familia yako ina furaha na ina umoja. Naamini ukimpa nafasi, utagundua Zainab ni msichana wa kipekee. Na kama baada ya miezi sita ya ndoa kupita hujamkubali, utakuwa huru kumuacha.”
Luqman alijikuta katika hali ngumu. Aliinama na kushika kichwa chake, alitafakari maneno ya mama yake. “Mama, hili ni jaribio kubwa sana la maisha yangu. Una uhakika gani? Kuwa Zainab ndiye mtu sahihi?”
“Nina uhakika japo sio sana,” Bi Naima alijibu kwa sauti ya kujiamini. “Na Sidrath pia anampenda sana. Fikiria hili kama fursa ya kujaribu kitu kipya na kuona kama kinaweza kufanya kazi. Najua wewe ni mgumu sana kuamini watu hasa wanawake”
Luqman aliendelea kutafakari kwa muda mrefu kabla ya kujibu. “Sawa, mama. Nitakubali, lakini naomba unipe muda kidogo wa kumfahamu vizuri kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.”
Bi Naima alitabasamu kwa furaha. “Asante, mwanangu. Umenifurahisha sana leo. Naamini mambo yatakuwa mazuri.”
Wakiwa wamezama kwenye mazungumzo, upepo wa usiku uliendelea kuvuma taratibu, ukishuhudia mwanzo wa safari mpya katika maisha ya Luqman. Ambae bado hakuwa na imani yoyote ile na huyo Zainab wao.
ITAENDELEA.....
SIMULIZI: MARRY MY DAD
MTUNZI: SUMAIYA MWENDO
SEHEMU YA : 05
Luqman Fafa alisimama mbele ya meza kubwa ya mbao iliyozungukwa na wanahisa wenye nyuso zilizokunjamana. Kikao kilikuwa kimejaa mvutano. Wote walikuwa wakijadili hasara kubwa iliyotokea kutokana na mradi wa uwekezaji uliokwama. Sauti za wanahisa wakitoa lawama zilijaza ukumbi huo wa kifahari.
"Luqman," mmoja wa wanahisa, Bwana Mungai, alisema kwa ukali, "Hatuku tarajia kuwa mradi huu ungefeli kiasi hiki. Tunahitaji maelezo ya kutosha ili kuelewa, na zaidi ya yote, tunataka hatua madhubuti ili kulinda uwekezaji wetu."
Luqman alitulia kwa muda, akiwatazama kwa macho makali. Kisha akasimama, alizungusha mkono wake kuonyesha ramani ya mradi kwenye skrini kubwa mbele yao. "Najua mko na hasira, na ni haki yenu. Lakini nataka muelewe jambo moja: mradi huu haujafeli. Tumekumbana na changamoto tu, ndiyo, lakini kila uwekezaji mkubwa una hatari. Na ni sisi pekee ndo tunaoweza kuubadilisha huu mradi uwe wa mafanikio makubwa zaisi licha ya changamoto kubwa tuliyoipata."
"Luqman, tunahitaji suluhisho, si hotuba!" mwanahisa mwingine, Bi Wanjiku, alikata kauli.
Luqman alitabasamu kwa upole lakini kwa kujiamini. "Suluhisho liko wazi. Tunahitaji kuongeza muda wa utekelezaji na kuzingatia zaidi masoko mapya. Tumeshakamilisha asilimia 70 ya kazi. Hatuwezi kurudi nyuma sasa. Kama hamtaki hasara kubwa zaidi, mnapaswa kuniamini."
Ukumbi ulinyamaza kwa sekunde kadhaa. Wanahisa walitazamana, wakibadilishana mawazo kwa macho. Hatimaye, Bwana Mungai aliisimama na kusema, "Sawa, Luqman, Kwa sababu mara zote umekuwa mtu imara na asie na kona nyingi katika kazi yako, Tutakupa nafasi ya mwisho. Lakini kumbuka, tunakutegemea."
Luqman alitabasamu kwa kweli afadhali walimuelewa. " Niwahakikishie tu ya kwamba hamtajutia." Wanahisa walielewa na kutoka nje japo kishingo upand3
☆☆☆☆
Baada ya kikao, Luqman alijisikia ni mwenye nguvu mpya. Alitoka ofisini huku akiwa kashika suti yake nyeusi ya gharama. Alipokuwa akielekea kwenye gari lake, alikutana na Abubakar, rafiki yake wa karibu.
"Luqman," Abubakar alimwita kwa sauti yenye furaha, "Nina njaa sana. Tafadhali, twende mahali popote nipate chakula kizuri."
Luqman alitabasamu. "Hii ni Nairobi, kila mahali kuna chakula kizuri. Lakini wewe pekee ndo unaejua wapi tunapaswa kwenda."
Abubakar alitafakari kwa sekunde chache, akatabasamu kimoyomoyo. Alimkumbuka Zainab na kuufikiria mgahawa wake wa kazi. "Twende pale kwenye mgahawa wa Cornerstone. Nafikiri utapenda chakula chao, pamoja na huduma zao zote."
" Mimi ni nani sasa hadi nikupinge wewe " Luqman alivuta midomo yake kwa tabasamu, kisha akafatana na Abubakar kuelekea kwenye gari, safari ikaanza moja kwa koja kwenda cornerstone.
Walipofika Cornerstone, mgahawa ulikuwa umejaa lakini ulionekana wa kuvutia zaidi.. Luqman alijitupa kwenye kiti huku akitazama mazingira kwa udadisi. Macho yake ghafla yakakutana na Zainab, ambaye alikuwa akihudumia wateja kwa uchangamfu wa hali ya juu.
Zainab alivaa sare safi ya mgahawa, nywele zake nyeusi nzuri sana na safi, zikiwa zimefungwa kwa ustadi kuelekea nyuma, na tabasamu lake liliangaza. Alizunguka meza kwa ustadi, akihakikisha kila mteja anahudumiwa vizuri. Luqman alibaki kumtazama kwa muda mrefu, alijjikuta akifikiria picha aliyotumiwa na binti yake, Sidrath, mara ya kwanza kabisa pamoja na zile picha nyingine alizopewa na Abubakar. Alimtambua mara moja kwamba huyo msichana alikuwa Zainab.
Alitafakari. "Huyu ndiye msichana ambae hata mama yangu anataka nimuoe?" aliwaza kimoyomoyo. Hakuweza kuondoa macho yake kwake. Hakika binti huyu ni mzuri sana jamani, macho yake, mashavu yake rangi ya ngozi yake, pamoja na tabasamu na uchangamfu wake. Aisee ni haki yao.kabisa kwa Sidi na bibi yake kumpenda kwa mara ya kwanza tu baada ya kumuona.
Zainab hakumwona Luqman, kwani alikuwa akihangaika na wateja wengi. Lakini baada ya muda, mhudumu mwingine, Fatina, alikuja kuwahudumia Luqman na Abubakar. Fatina alionekana mchangamfu lakini aliyechanganyikiwa kidogo kutokana na msongamano wa wateja.
Fatina alipokuwa akiweka bakuli la mchuzi mezani kwa Luqman, mkono wake uliyumba kidogo, na mchuzi ukamwagika moja kwa moja kwenye suti ya Luqman.
"Oh my God!" Fatina aliguna kwa hofu, akaanza kuomba msamaha. "Samahani sana, sikukusudia!"
Luqman alisimama kwa ghafla, uso wake ukiwa umejaa hasira. "Unajua hii suti inagharimu kiasi gani? Uzembe wako haukubaliki kabisa!" Alimfokea kwa sauti kubwa.
Fatina alitetemeka, machozi yalianza kumtoka kwa hofu na uwoga. "Naomba msamaha, bwana. Naomba unielewe pia haikuwa nia yangu niamini tafadhali..."
Alipokuwa akiendelea kuomba msamaha, Zainab aligeuka na kualiangalia kilichokuwa kikiendelea kutoka upande mwingine wa mgahawa. Aliona jinsi Luqman alivyomsukuma Fatina kwa hasira. Hakuweza kuvumilia kuona mwenzake akidharauliwa hivyo.
Zainab alisogea haraka, akamuinua Fatina kutoka sakafuni na kumkumbatia ili kumpa faraja. Kisha akamkabili Luqman moja kwa moja, uso wake ukiwa umejaa hasira.
"Bwana, hata kama umekosewa, huna haki ya kumfanyia hivi mwanamke alafu we si wa kiume wewe?. Ungeweza kuelewa na kumpa moyo tu kama binadamu aliekosea, lakini badala yake unamnyanyasa. Huo siyo utu!" Zainab alisema kwa sauti ya uthabiti.
Luqman alimwangalia Zainab kwa mshangao. "Na wewe ni nani hadi unifundishe namna ya kuwa na adabu? Msichana asiye na adabu kabisa!" alijibu kwa ukali.
" Asie na adabu ni wewe mwanaume gani unamsukuma mwanamke, ki ufupi nina mashaka makubwa sana wewe"
Luqman alichukia anawezaje kuushuku uanaume wake?
Maneno hayo yaliamsha ugomvi mkubwa kati yao, huku Zainab akimtetea Fatina kwa nguvu zote, na Luqman akisisitiza kwamba hakuwa na kosa kwa hasira yake. Abubakar, aliyekuwa ametulia kimya, alishika kichwa chake kwa mkono mmoja, akihisi kizunguzungu kutokana na hali hiyo. Alikuwa amekuja hapo na Luqman akiwa na nia ya kuwaunganisha Luqman na Zainab, lakini sasa aliogopa kwamba huenda mpango wake hautakaa ufanikiwe hata kidogo.
ITAENDELEA........
SOMA MAELEKEZO
Bonyeza hi "Soma Kitabu" kisha itakupeleka kwenye fomu yaku login, hakikisha ume login na namba uliyojiunga nayo ndipo utaendelea sasa kusoma kitabu chote